The House of Favourite Newspapers

Okwi aivuruga Simba, ajiondoa!

MSHAMBULIAJI wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, kama kawaida yake ameanza kuonyesha ‘pozi’ kwa timu hiyo, baada ya kujiondoa kikosini huku Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini ‘Sauzi’ ikitajwa kuhusika.

Hiyo, ikiwa ni saa chache baada ya timu hiyo ianze safari ya kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC uliopigwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani huko.

 

Mganda huyo, hivi sasa ni anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine kwa mujibu wa kanuni za usajili za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambazo mchezaji akibakiza miezi sita katika mkataba wake huku ule wa Okwi ukitarajiwa kumalizika Aprili 26, mwaka huu.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Okwi aliachwa kwenye msafara wa timu uliokwenda Morogoro kucheza na Mbao huku benchi la ufundi la timu hiyo likiongozwa na Mbelgiji, Patrick Aussems likiwa halina taarifa yoyote.

 

Mtoa taarifa huyo alisema, mshambuliaji huyo alianza vituko na pozi kwa timu hiyo kwenye michezo ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika walipocheza michezo ya marudiano na JS Saoura, AS Vita na baadhi ya michezo ya ligi huku sababu akielezwa majeraha ya enka.

 

Aliongeza kuwa, uongozi ulishtuka kumuona Okwi akiripoti kwa wakati kwenye kambi ya Uganda iliyokuwa inajiandaa na mchezo wa kufuzu Afcon na Taifa Stars hali inayowapa maswali mengi mabosi hao ya kutoelewa nini kinaendelea kwa nyota huyo.

 

“Tangu timu imeanza maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya Mbao FC, Okwi hajaonekana mazoezini wala kambini, pia hayupo kwenye msafara wetu wa timu uliosafiri kwenda Morogoro.

 

“Benchi la ufundi halina taarifa yoyote yake wakati Juuko (Murshid, raia wa Uganda) yeye tangu mazoezi ya kwanza yupo kambini na amefanya mazoezi, hivyo tunashangaa labda yupo kwenye mipango yake ya kutaka kuondoka kwenda Sauzi.

 

“Kocha hivi sasa amemuondoa kwenye mipango yake ya mchezo wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya TP Mazembe kutokana na utovu wake wa nidhamu ambao ameuonyesha, akiamini bila ya yeye timu ina uwezo wa kupata matokeo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Aussems kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Mimi sina taarifa yoyote ya Okwi, labda viongozi kwani tangu kwenye mazoezi ya siku ya kwanza hakuwepo hadi ya mwisho tuliyofanya jana (juzi) jioni hakuwepo.

 

“Hivyo, sifahamu chochote mimi hivi ninaangalia wachezaji hawa niliokuwa nao katika timu pekee kwa kuanzia mchezo huu wetu wa ligi dhidi ya Mbao na ule wa kimataifa dhidi ya TP Mazembe (Jumamosi ijayo), ninaamini hawa wachezaji niliokuwa nao watatupa matokeo mazuri.

” Kwa upande wa meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alisema:

 

“Mimi sijui chochote cha kuhusiana na Okwi labda ya viongozi wangu wa juu, hayupo kwenye msafara wetu huu unaoelekea Morogoro, hivyo waulizwe viongozi wa juu suala hilo.”

 

Okwi, inaelezwa hivi sasa yupo kwenye mazungumzo na Orlando Pirates inayowania saini yake katika usajili wa msimu huu wa ligi ya nchini huko. Simba, Jumamosi ijayo itacheza mechi ya kwanza ya robo fainali na TP Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

 

Jana, Simba iliingia dimbani na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu baada ya kuichapa Mbao FC kwa bao 3-0.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam.

Comments are closed.