The House of Favourite Newspapers

Okwi Alivyoishusha Yanga Kileleni

0

SAA 24 tangu Yanga ipande kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuifunga Kagera Sugar, juzi Jumamosi, hatimaye wapinzani wao wa jadi, Simba wakabadili msimamo wa ligi hiyo kwa kuwashusha na kurejea kileleni licha ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliopigwa jana Jumapili.

Simba ambayo ilipata wakati mgumu kusawazisha bao katika mchezo huo wa jana, sasa inalingana pointi na Yanga lakini yenyewe ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ambapo ina wastani wa mabao 11 wakati Yanga ina wastani wa mabao 3 sawa na Mtibwa Sugar ambayo nayo ina pointi 12 sawa na vigogo hao wa juu.

Katika mchezo huo wa jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Mtibwa ndiyo ambayo ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 36 kupitia kwa Stamili Mbonde ambaye alifunga kwa kichwa baada ya walinzi wa Simba kuzubaa wakati mpira wa kona ulipopigwa.

Baada ya hapo mchezo ulikuwa mkali na Simba ililazimika kuongeza nguvu ya ziada kuweza kusawazisha bao hilo katika dakika ya 94, ikiwa ni katika dakika za nyongeza baada ya zile 90 za kawaida kukamilika.

Emmanuel Okwi alifunga bao hilo kwa njia ya faulo iliyotokana na mchezaji wa Simba, Erasto Nyoni kuchezewa faulo na Casian Ponela nje kidogo ya eneo la 18 la Mtibwa Sugar.

Aidha, katika mchezo huo, Simba iliwapoteza wachezaji wake John Bocco na Salum Mbonde ambao wote waliumia katika nyakati tofauti na nafasi zao kuchukuliwa na Juma Liuzio na Juuko Murshid, pia kiungo Shiza Kichuya alitolewa katika mchezo huo kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla.

Katika mchezo mwingine, Tanzania Prisons ililazimishwa suluhu na Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mwandishi Wetu, Dar na Derrick Lwasye, Mbeya  

Leave A Reply