The House of Favourite Newspapers

Hospitali ya Aga Khan Lazima Ibadilike, Vinginevyo Itaendelea Kuchafua Sura ya Kiongozi Wao wa Dini

0

 

WIKI iliyopita nilielezea namna ambavyo nilimpeleka mama yangu Hospitali ya Aga Khan kutibiwa akiwa na tatizo la shingo (Spondylosis), miguu, matatizo ya moyo na na figo, ambayo kwa kweli amekuwa nayo kipindi kirefu sasa na huwa anatibiwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo Aga Khan.

Hali yake haikuwa mbaya sana, ma ana ba ada y a daktari bingwa (Dr Mohamed) kumuona, alisema achukuliwe tu vipimo kisha arejee nyumbani na nimpeleke tena siku iliyofuata baada ya majibu kutoka na pia aweze kuonwa na daktari bingwa wa upasuaji wa mishipa ya fahamu, Dr Mugisha, hii inaashiria kabisa kwamba hali ya mama yangu haikuwa mbaya, hakustahili kulazwa.

Kwa kuwa mama yangu ameugua muda mrefu na hapendi sana kwenda hospitali, nilimshauri daktari akubali, ingawa malipo ya kitanda katika Hospitali ya Aga Khan ni Sh. 150,000 kwa siku, sawasawa kabisa na hoteli ya kitalii, akubali mama alazwe wodini hapo hadi siku iliyofuata majibu yakitoka ili apate matibabu, hali ya mama yangu ilikuwa nzuri, tulikuwa tukiongea kawaida na alikuwa anakataa kulazwa, shinikizo lake la damu lilikuwa 120/80mmHg, la kawaida kabisa.

Mimi na dada yangu, Lydia tulimbembeleza sana hadi akakubali kulazwa, nikaondoka kurejea nyumbani, siku iliyofuata majibu yalipotoka yalionesha madini ya chumvi (Sodium) yalikuwa yameshuka hadi kiwango cha 115mEq/l, wakati kawaida huwa ni 135mEq/l.

Nilipata nafasi ya kukutana na daktari ambaye alisema kiwango hicho cha Sodium kilikuwa ni hatari, yeye alikiita Critically Low, yaani ilikuwa chini mno na ingeweza kusababisha matatizo, mtu akiwa na madini ya chumvi kidogo kwenye damu, miongoni mwa matatizo ambayo humpata ni pamoja na kuchanganyikiwa na shinikizo la damu kushuka.

Daktari aliandika mama yangu apewe dawa iitwayo Hypertonic Saline, ambayo huwa ina madini ya chumvi 3%, hutolewa kwa mgonjwa aliyepungukiwa madini hayo ili kuyapandisha, mama alishafanyiwa matibabu haya mara kadhaa huko nyuma katika hospitali hiyohiyo! Moyoni tukawa na faraja kwamba tatizo lilikuwa limepatiwa tiba, tukabaki tukisubiri awekewe dripu ya dawa hiyo, lakini hakuwekewa hadi siku iliyofuata, shinikizo la damu likawa limeshuka hadi 90/50mmHg, karibu kabisa na kifo!

Sikuelewa ni kwa nini wauguzi walikuwa hawamwekei dawa ambayo tayari ilishaandikwa kwenye faili, wakati hali ilikuwa imezidi kuwa mbaya, sasa mgonjwa aliyekuwa akiongea, akawa haongei tena na mipango ya kumpeleka chumba cha wagonjwa mahututi ikaanza!

Siwezi kuficha, kufikia hapo nilianza kupotez a uvumilivu, nikataka niitiwe daktari, alipokuja niliongea naye, akaanza kunieleza maneno ambayo kwangu mimi hayakuleta maana, eti walikuwa wameamua badala ya kumpa hiyo dripu, wangepunguza tu maji yanayoingia mwilini kwa sababu upungufu wake wa madini ya chumvi ulisababishwa na maji kuzidi kwenye damu, hali iitwayo kwa kitaalam Haemodilution!

Kwangu mimi aliyoyasema daktari hayakuniingia kichwani, kwa akili ya kawaida tu alichokisema kisingeweza kusaidia! Nikaanza kuhisi, ninaweza kukosea kama binadamu, kwamba kulikuwa na mchezo uliokuwa ukiendelea wa kuhakikisha mama yangu anafika chumba cha wagonjwa mahututi, lakini mwisho wa siku gharama ya matibabu iwe kubwa.

Nilipata hisia hizi kwa sababu ninaifahamu Aga Khan, hospitali inayoendeshwa na shirika la dini, kwa sababu hiyo hailipi kodi yoyote, lakini gharama zake za matibabu huwa ni kubwa kupindukia, kuzidi hata hospitali binafsi zinazolipa kodi kama vile Regency na nyinginezo.

Nimekwisha shuhudia miili ya wagonjwa walioaga dunia ikikataliwa na hospitali hadi ndugu wa marehemu walipe mamilioni ya fedha wanazodaiwa, hivi leo ninavyoandika makala hii Oktoba 14, Siku ya Mwalimu Nyerere, kuna mgonjwa amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi na gharama ya matibabu imekwishafika Sh. Milioni 60, familia inachanganyikiwa, wamekwishachangishana hadi wamechoka.

Uamuzi nilioufikia ni kuutafuta uongozi wa hospitali, nikaoneshwa mahali ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi ilipo, hapo nilikutana na mama mmoja mpole na mtaratibu, jina lake ni Mama Hwai, nikamweleza kila kitu kilichotokea, akasikitika mno na kusema angefuatilia baada ya muda mfupi akitutaka mimi na mke wangu turejee wodini.

Muda mfupi baadaye, mama alihamishwa wodi ya kawaida na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi, akiwa hajitambui, shinikizo la damu liko chini, wanahangaika kulipandisha! Hebu fikiria, umempeleka mama yako hospitali akiwa anaongea, sasa hali yake imekuwa mbaya, akiwa kwenye hospitali kubwa kama Aga Khan, ‘hai-make sense’ hata kidogo.

Kitu kingine kibaya kabisa, Hospitali ya Ag a Kh a n  walishagoma kabisa kutumia kadi ya Bima ya Afya (NHIF) kwenye hospitali yao kubwa, yenye vifaa, maana yake hapa ni kuwatenga Watanzania wenye kipato kidogo na kukumbatia matajiri! Wakati Aga Khan inafanya haya, hailipi kodi hata kidogo kwa Mtanzania, ninaamini utajiri mkubwa inaotengeneza kwenye huduma za afya ndiyo unaoiwezesha kufanya uwekezaji mwingine mkubwa.

Tukiwa nje ya chumba cha wagonjwa mahututi, niliitwa na kuingia ndani, huko nilikutana na jopo la madaktari tukaingia kwenye mjadala wakijaribu kunieleza kilichotokea, kifupi walikuwa wakijaribu kwa njia ya mzunguko kuniomba msamaha kwa uzembe uliofanyika wodini ambao sasa ulitaka kugharimu maisha ya mama yangu.

Mwisho kabisa waliahidi wangepambana kufa na kupona kuokoa maisha ya mzazi wangu, sikuwa na maneno mengi ya kusema, nilichohitaji ni mama yangu apone, muda wote nilikuwa nikimwomba Mungu kimoyomoyo kwani yeye ndiye mponyaji!

Siku iliyofuata, hali ya mama yangu baada ya kuwekewa dripu aliyotakiwa kuwekewa wodini, ilikuwa imerejea katika hali ya kawiada, shinikizo la damu lilikuwa sawasawa na chumvi ya damu ilikuwa imeongezeka ikielekea kwenye kawaida.

Akahamishwa chumba cha wagonjwa mahututi na kupelekwa wodi ya kawaida, shukurani nyingi sana ziwaendee madaktari wa chumba cha wagonjwa mahututi, bila wao ningempoteza mama yangu! Siku chache baadaye aliruhusiwa kutoka hospitalini, gharama ya matibabu ikiwa Sh. Milioni 5! Niulize dawa alizopewa, hakuna zaidi ya dripu ya Hypertonic Saline, dawa za moyo, dawa za kuua wadudu, zilizobaki zote ni vipimo na gharama ya kitanda!

Hivyo ndivyo ilivyo katika hospitali nyingi hapa nchini, wagonjwa wanarundikiwa vipimo hata visivyohitajika, unaweza kupimwa kipimo kilekile mara nne kwa siku! Ushahidi ninao, wanapofanya hivi kwa shirika la bima huwa inaonekana kama ni sawa, kwani mashirika ya bima yanazitajirisha hospitali binafsi usiku na mchana, ni Shamba la Bibi, tatizo linakuja pale ambapo mgonjwa analipa fedha taslimu kama ilivyokuwa kwangu pale Aga Khan.

Niliondoka nikiwa nimechukia sana moyoni mwangu, tafsiri ilikuwa ni kwamba mgonjwa wangu al ipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi ili tu nilipe fedha nyingi! Hakika sifichi, nilipiga simu sehemu nyingi sana hapa nchini kutoa malalamiko yangu, hakuna sehemu muhimu ambako sikupiga simu kupinga vitendo vya aina hii ambavyo watu wanafanyiwa.

Wapo watu wengi sana wana malalamiko juu ya Hospitali ya Aga Khan, lakini wanaogopa kusema, kwamba wanaweza kupata matatizo siku wakirejea tena hospitalini hapo kutibiwa, mimi nimeamua kuj i toa mhanga litakalokuwa na liwe. Nikiugua leo bado nitakwenda hapohapo Aga Khan kutibiwa, wakigoma kuni t ibu kwa sababu tu nilifungua mdomo kusema ukweli, sheria zipo.

Siku moja baadaye nilisoma gazetini kwamba Kiongozi wa Madhehebu ya Ismailia Duniani, Mtukufu Aga Khan, ambaye ndiye pia mmiliki wa Hospitali ya Aga Khan na vitegauchumi vingi duniani, alikuwa anatembelea Tanzania, Oktoba 11, nikasema enhee! Sasa huu ndiyo wakati sahihi wa kumfikishia ujumbe Mtukufu Aga Khan juu ya yanayoendelea kwenye taasisi zake, maana inawezekana kabisa yeye kama mtumishi wa Mungu anafichwa, watu wanachafua jina lake, pengine bila yeye kufahamu.

Nikaamua kwa siri kubwa bila kumshirikisha mtu yeyote zaidi ya katibu muhtasi wangu, Glory Masawe, kuandaa bango linaloonekana kwenye picha ili niende nalo uwanja wa ndege kumpokea, moyoni mwangu nilijua Rais John Magufuli angekuwa pale na angemuuliza Aga Khan swali kwa nini hospitali yake kuu haikubali kuhudumia wagonjwa wa bima ya taifa ya afya, wakati hatulipi kodi yoyote?

Je, nini kilitokea uwanja wa ndege? Fuatilia.

Kumbukumbu za Kweli za Maisha Yangu-214, ERIC SHIGONGO

Leave A Reply