The House of Favourite Newspapers

OLE Shtuka Watakugeuka Man UTD, Watakufukuza

WAKATI Alex Ferguson anajiandaa kustaafu soka mwaka 2012 aliukosa ubingwa dakika za mwisho tena kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya wapinzani wake wa jiji moja, Manchester City.

 

Inaelezwa kuwa Ferguson alipanga kuondoka mara baada ya kukamilisha mchakato wa kutwaa ubingwa wa Premier League, ili aiache Manchester United ikiwa na heshima kubwa na ikiwa kileleni, bahati mbaya hilo likashindikana.

 

Alisogeza mbele zoezi lake la kustaafu kwa kuwa aliona alipokuwa amekosea, ana moyo wa ujasiri, akaamua kupambana ili lengo lake la kuondoka kwa heshima litimie.

 

Akamsajili Robin Van Persie na kuongeza nguvu kwenye kiungo kwa kumsajili Shinji Kagawa. Alitambua kuwa kikosi chake kilikuwa kwenye kilele cha mafanikio lakini alichokosa ni mtu wa mwisho wa kufanya kazi ya kufunga inavyotakiwa.

Kwa asili ya Premier League huwezi kuwa bingwa kama huna straika wa maana anayejua kufunga, iwe ni mmoja au wawili lakini lazima unapokuwa na straika ambaye anakupa uhakika wa kufunga zaidi ya mabao 20 kwa msimu mmoja basi unakuwa na uwezo wa kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

 

Ferguson alilijua hilo, ndiyo maana alichokifanya Van Persie kilithibitisha kile ambacho alikuwa akikitaka kocha huyo, akabeba ubingwa kirahisi tena kwa tofauti kubwa ya pointi, akastaafu.

 

Mashabiki wengi wa Man United waliamini historia itaendelea, lakini ukweli ni kuwa kocha huyo aliiacha timu ikiwa inaelekea ukingoni mwa mafanikio, na kocha aliyefuata alitakiwa kulitambua hilo na kuanza kuijenga timu taratibu, badala yake David Moyes akaamini amerithi kikosi bora.

Moyes alipata wakati mgumu kwa kuwa wachezaji waliokuwepo walikuwa wakielekea ukingoni mwa ubora wa juu wa soka lao, wengine walikuwa wameshashinda mataji mengi na hivyo walikosa ile hamasa ya kufanya kitu cha ziada, hapo ndipo Man Unite ilipotakiwa kuanza kujengwa upya.

 

Mabosi hawakulitambua hilo, waliendelea kuishi na historia, na ndicho kitu ambacho kinawatesa kwa kuwa imewachukua muda mrefu kutambua hilo.

Mzigo ulikuwa mkubwa sana kwa Moyes, kwa faida ya kulinda nembo ya klabu ikabidi afukuzwe.

Alipochukuliwa Louis van Gaal, walitambua ni kocha mkongwe ambaye anaweza kutumia uzoefu wake kuanza kujenga timu wakati ikijiandaa.

 

Bahati mbaya Van Gaal akakutana na kipindi ambacho ili uwe bingwa lazima uwe utumie nguvu kubwa kusajili, biashara ya kuanza kutengeneza kikosi wakati presha ni kubwa klabuni hapo ukawa mzigo mkubwa mwisho naye akatimuliwa.

Walipofukuzwa makocha hao siyo kwa kuwa walikuwa ni wabovu, bali kwa kuwa walishindwa kuendana na uhalisia wa nini hasa kinatakiwa, viongozi waliwadanganya kuwa watawapa muda wa kuunda timu lakini presha ikizidi wao makocha ndiyo wanabebeshwa lawama.

 

Kuajiriwa kwa Jose Mourinho ilikuwa ni mipango ya muda mfupi ili kurejesha heshima ya mataji, kwa kuwa inajulikana wazi kocha huyo siyo mzuri kwenye kukuza vipaji bali anaweza kutumia fedha kutengeneza timu ambayo inaweza kupigania mataji.

 

Naamini haya viongozi wenyewe wa Man United wanajua ajira ya Mourinho ilikuwa ni mpango wa muda mfupi, kwani kiasi fulani alifanikiwa lakini kilichomponza baadaye ni kuwa alishindwa kuishi na kizazi cha sasa cha soka.

 

Enzi Mourinho anatamba Porto, Chelsea na Inter Milan, makocha walikuwa na nguvu kubwa kuliko wachezaji, lakini sasa hivi mambo ni tofauti na ndiyo maana vita yake na Paul Pogba ilichangia kocha huyo kufukuzwa.

 

 

Ujio wa Ole Gunnar Solskjaer ni sahihi, lakini kiuhalisia uongozi ulichelewa kufanya maamuzi ya kumpa mtu wa aina yake.

Ole ni kocha ambaye anaijua vizuri United, lengo lake ni zuri, kuitengeneza United kuanzia chini kama alivyofanya Ferguson ili baadaye awe na ufalme wake, yaani wachezaji wamuelewe na waishi vile kocha anavyotaka kama ilivyokuwa enzi za kocha wake wa zamani.

 

Kumbuka kuwa wakati Ferguson anafanya yote hayo, presha ilikuwepo lakini siyo kubwa kama ilivyo sasa, nembo ya klabu ni kubwa mara 1000 zaidi ya ilivyokuwa wakati Ferguson akipambana kuitengeneza timu.

 

Inawezekana Ole anatambua kuwa uongozi chini ya Ed Woodward unaelewa anachokifanya lakini kwa mazingira ya uhalisia wa sasa nina hofu kuwa mambo yataenda ndivyo sivyo.

 

Man United ya sasa haina levo hata nusu ya United ambayo imesababisha zaidi ya watu bilioni kadhaa kuipenda timu hiyo, huo ndiyo uhalisia.

 

Kabla ya kuanza kwa msimu huu, nilimwambia rafiki yangu mmoja kuwa naiona United ikiwa na anguko kubwa uwanjani kwa kuwa haina straika.

Akaniambia wanaye Marcus Rashford, nikamwambia huwezi kupigania ubingwa Premier League ukiwa na straika mwenye levo za Rashford, ni mchezaji mzuri lakini mzigo wa kuibeba timu hiyo tena wakati huu ambapo ipo kwenye kipindi cha mpito ni mkubwa na kwa kijana kama yeye hawezi kuubeba.

 

Juzi baada ya kufungwa na Newcastle United, David de Gea, kipa mkongwe wa United alitoa kauli ambazo zinaonyesha wazi kuna tatizo klabuni hapo.

Alisema wamekuwa wakionyesha kiwango kibovu tangu kuanza kwa msimu huu, na inavyoonyesha bado hawajajua tatizo lakini watapambana.

 

Upande wa Ole kila akiulizwa kauli yake ni ileile, wachezaji hawajitumi na watapambana, lakini uhalisia ni kuwa wachezaji waliopo sasa kikosini hapo hawana ubora wa kuwa washindani wa ubingwa.

 

Sasa hivi uongozi upo nyuma ya Ole kwa kuwa unatambua hakufanya usajili mkubwa hasa kuanzia kwenye kiungo na ushambuliaji, na lengo lao ni kumpa muda ili aitengeneze United anayoitaka.

 

Lakini kipigo katika mchezo ujao dhidi ya Liverpool au vikiendelea kwenye mechi kadhaa zijazo, upepo utabadilika na hakuna atakayekumbuka kuwa hakusajili au anajenga timu, Atafukuzwa.

 

Uhalisia ni kuwa United ina mzigo mzito wa kufanya mabadiliko kama kweli inataka kuishi kwenye hadhi ya jina

lake.

MAKALA NA JOHN JOSEPH

Comments are closed.