OMBA, SALI UMPATE MUME MWENYE TABIA HIZI 6!

WIKI hii nitazu-ngumzia sifa 6 za mwanaume ambaye anastahili kuwa mumeo. Nafanya hivi ikiwa ni msaada kwa wale ambao wamefikia hatua ya kuingia kwenye ndoa lakini bado wanashindwa kutambua yupi ni sahihi na yupi si sahihi kuitwa mume.  Tufahamu kwamba si kila mwanaume unayekutana naye na ukampenda anafaa kuwa mumeo. Wengine wana mapungufu makubwa ambayo bila kuyabaini na ukaingia kichwakichwa, utakutana na matatizo makubwa.

Wito wangu kwako wewe msomaji ni kuhakikisha unaomba na kusali sana ili kuhakikisha unampata mume mwenye sifa nitakazozitaja hapa chini;

ANAKUPENDA KWA MAANA YA KUKUPENDA

Unapoingia kwenye maisha ya ndoa, unatarajia kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwenza wako. Wapo wanaume ambao wanaonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga.

Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na demu flani bomba au kuonja tu penzi kisha kuanza visa ili muachane. Kwa nini ni vizuri kumpata mwanaume mwenye mapenzi ya dhati? Hii inatokana na ukweli kwamba kinyume na hivyo, maisha yatakuwa ya migogoro kila siku.

TABIA

Linapokuja suala la ndoa, tabia inakuwa kitu cha awali sana kuangaliwa. Hii ni kwa sababu, wapo wanaume ‘handsome’, wenye kazi nzuri na kipato kizuri lakini wanakosa sifa ya kuitwa mume kutokana na tabia zao chafu.

Hakuna mwanamke anayeweza kudiriki kumpa nafasi mwanaume kuwa mume wake wakati ana tabia chafu. Endapo utaangalia uzuri wa sura kisha ukafanya maamuzi ya kuolewa naye, utakuwa umejichimbia kaburi.

YEYE NA MAFANIKIO

Mwanaume anatakiwa kuwa dereva katika safari ya kusaka mafanikio, sasa kama atakuwa ni mtu wa kukaa kijiweni, kupiga mizinga, mvivu asiyependa kujishughulisha kwa namna yoyote, huyu hafai kupewa nafasi ya kuitwa mume.

Ile dhana ya kukubali kuolewa na mwanaume yoyote ili mradi upate heshima ya kwamba umeolewa, imepitwa na wakati. Mwanaume sahihi ni yule mwenye malengo maishani, anayefikiria nini cha kufanya kwa ajili ya maendeleo yake, mkewe na watoto wao.

WA SHIDA NA RAHA

Wapo wanaume ambao sio wavumilivu kabisa katika maisha.Tunajua maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha. Kwa mfano, unaweza kuingia kwenye maisha ya ndoa lakini kwa bahati mbaya ukawa huna kizazi, mwanaume mwenye mapenzi ya kweli na wewe anatakiwa kukuvumilia na kuwa upande wako.

Yule ambaye atakuwa anaungana na dada zake kukushambulia kwa kutozaa, hafai kuwa na wewe kwani yapo mengi yanayoweza kutokea yanayohitaji kuvumiliana. Kimsingi uvumilivu kwa mwanaume utakuwepo kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali.

ASIE NA TAMAA ZA KIJINGA

Wanaume wenye tamaa za kijinga ndiyo ambao wakishaingia kwenye maisha ya ndoa wanakuwa wepesi kusaliti. Hao hawastahili kuitwa waume za watu. Ni hayo kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.


Toa comment