The House of Favourite Newspapers

Pasi za Tambwe zazua balaa jipya Simba SC

0

AmissTambwe2

Mshambuliaji  wa Ynga, Mrundi, Amissi Tambwe.

Sweetbert Lukonge,Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amezua balaa jipya katika Klabu ya Simba baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Muingereza, Dylan Kerr, kuhoji kwa nini aliondoka klabuni hapo.

Kerr alifikia hatua hiyo baada ya kumshuhudia Tambwe katika runinga akiiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wake wa ufunguzi wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union ya jijini Tanga.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tambwe ndiye aliyetoa pasi za mwisho kwa wafungaji wa mabao hayo ambao ni Simon Msuva na Donald Ngoma.

Akizungumza na Championi Jumatano, kiongozi mmoja wa juu wa Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake, alisema Kerr baada ya kumshuhudia Tambwe akiwatengenezea wachezaji wenzake nafasi hizo za mabao, alihoji na kutaka kujua sababu iliyoifanya Simba iachane naye.

“Nilipomwambia sababu yenyewe alisikitika sana kwani alidai kuwa tulimuacha mchezaji mzuri ambaye kama msimu huu angekuwepo kikosini, basi angekuwa na msaada mkubwa sana katika kikosi chake.
“Alisema Tambwe ni mchezaji asiye na mambo mengi uwanjani na anajua kazi yake vizuri kuwa anatakiwa afanye nini na kwa wakati gani,” alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, Kerr alipoulizwa kuhusiana na jinsi alivyomuona Tambwe katika mchezo huo, alisema: “Ni mchezaji mzuri lakini kwa sasa siwezi kumzungumzia kwa sababu hayupo kwenye kikosi changu.”

Simba iliachana na Tambwe msimu uliopita baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri, kudaiwa kuwa ndiye aliyependekeza afungashiwe virago vyake klabuni hapo kwa madai kuwa kiwango chake kimeshuka.

Leave A Reply