The House of Favourite Newspapers

Peneza Amvaa Polepole Aliyesema Viti Maalumu Chadema ‘Wamepitiwa’ na Mbowe

MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza,  amemvaa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphery Polepole, kuwa amewadhalilisha wabunge wa viti maalumu wanaotokana na chama chake kuwa wamepata nafasi hizo baada ya kufanya ngono na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

 

Peneza ameyasema hayo jana Jumatano Aprili 17, 2019, akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2019/20.

 

“Mwenyekiti na viongozi wengine wa Bunge walikemea tabia hii ya kipuuzi, lakini sasa imefika huko nje ambapo ndugu Humphrey Polepole amesema wabunge wa viti maalum wa Chadema wanapatikana mpaka ‘wapitiwe’ na mwenyekiti wao, huu ni udhalilishaji.

 

“Sasa kama hata hatambui haki za kikatiba ni aibu kwa Chama Cha Mapinduzi kuwa na mwenezi anayedhalilisha wanawake… lakini ifike mahali nafasi walizonazo na vyeo walivyonavyo viheshimiwe,” amesema akisisitiza kwamba ni aibu kwa kiongozi kusimama na kusema kuwa nafasi ya mwanamke kisiasa inatokana na ngono.

 

“Ni aibu kwa kiongozi wa nchi hii kusimama na kusema kwamba mafanikio ya mwanamke ya kisiasa yanatokana na shughuli za kingono.  Tunawajengea watoto wetu fikra mbaya ndani ya vichwa vyao,” amesema Peneza.

Comments are closed.