The House of Favourite Newspapers

Penzi Lenye Maumivu-6

0

ILIPOISHIA IJUMAA… Alitamani kumkatalia, lakini wakati mwingine hakuona kama hilo lilikuwa jambo jema kwani hata yeye mwenyewe mwili wake ulikuwa kwenye msisimko mkubwa, hakukuwa na kitu kingine alichokuwa akikihitaji kama kuwa kwenye uhusiano na mwanaume. SONGA NAYO…

USIKU huo hakulala, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Wilbert, alijaribu kupanga maneno ya kumwambia mvulana huyo kama tu angehitaji kuwa mpenzi wake. Usiku huo saa zilionekana zikikatika kwa haraka sana, hakujiamini, hakujua kama angeweza kusimama mbele ya mvulana huyo na kuzungumza naye.

Siku hiyo alilala saa sita usiku, asubuhi ilipofika, alijiandaa na kwenda shuleni. Ndani ya gari, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, dereva wake alimshtukia, hakuonekana kuwa kawaida kama siku nyingine, akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, akamuuliza, lakini Halima hakumwambia ukweli, alimpa sababu nyingine kabisa.

“Sijisikii vizuri, ninahisi mwili kuchoka sana,” alisema Halima.

“Kweli?”

“Niamini Andrew. Nimechoka sana,” alijibu Halima.

Hakuwa amechoka, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Wilbert tu. Alipofika shuleni, moja kwa moja akaelekea darasani. Alitaka kumuona mvulana huyo, alitaka kujua alifananaje, alikuwa na muonekano upi na alikuwa na uzuri gani.

Ulipofika muda wa mapumziko, huku akiwa amesimama nje ya jengo la kula chakula, Wilbert alimsogelea Halima, alipomfikia, akamsalimia kwa kumpa mkono. Bila shaka Halima akajua kwamba huyo ndiye alikuwa Wilbert mwenyewe, akasalimiana naye.

“Umependeza sana leo, unaonekana mzuri zaidi ya siku nyingine,” alisema Wilbert huku akimwangalia Halima, uso wake ulikuwa na tabasamu tele.

“Ahsante!” Alijibu Halima huku naye akirudisha tabasamu pana.

“By the way, naitwa Wilbert Kinyambi,” alisema Wilbert.

“Naitwa Halima Hawadhi.”

Japokuwa alionekana kujiamini, lakini Wilbert alikuwa na hofu kubwa moyoni mwake. Alitetemeka, hakuamini kama kweli alisimama na Halima, msichana aliyekuwa akimpenda kuliko wasichana wote shuleni hapo.

Walizungumza mambo ya kawaida, kutokana na hofu aliyokuwa nayo, yale maneno yote aliyokuwa amepanga kuzungumza na msichana huyo yakapotea kabisa. Kitendo cha yeye kusimama na msichana huyo, kila mtu akaanza kumwangalia kwa wivu uliochanganyikana na macho ya chuki.

Kila mtu alimpenda Halima, alikuwa msichana mrembo ambaye hakuwahi kutokea shuleni hapo, wengi walijaribu kumfuatilia, lakini tatizo ni kwamba msichana huyo hakuwapa nafasi ya kuzungumza nao, walipoona Wilbert amepata nafasi hiyo, mioyo yao iliumia mno.

Huo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, wakawa wakizungumza mara kwa mara. Wakawa wanapigiana simu na kujuliana hali, lakini hakukuwa na yeyote ambaye alimwambia mwenzake ukweli kwamba alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

Wakati huo walikuwa kidato cha tatu, siku zikakatika, wakaingia kidato cha nne, ukaribu wao uliendelea kuwa hivyohivyo, walipendana na kuthaminiana na katika kipindi chote hicho hakukuwa na yeyote aliyemwambia mwenzake kwamba alikuwa akimpenda.

Baada ya siku kusonga mbele na kubaki mwezi mmoja kabla ya kumaliza kidato cha nne, Wilbert hakutaka kuvumilia, aliishi na Halima kama dada yake au ndugu yake, hakutaka kuona hilo likiendelea, alichokifanya ni kujipanga kwa ajili ya kumwambia msichana huyo ukweli wa moyo wake, kama kuvumilia, alivumilia sana na alichoka hivyo akajipanga.

Siku hiyo aliyopanga kuonana naye, alishindwa kuvumilia na aliona siku hiyo ndiyo kuwa nafasi hiyo adimu aliyokuwa akiihitaji katika maisha yake. Akampigia simu msichana huyo na kumwambia kwamba alitaka waonane.

“Kuna kitu?”

“Ndiyo! Kikubwa tu, naomba tuonane Halima,” alisema Wilbert kisha akakata simu.

Hakutaka kukubali, alitamani kumwambia kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya kuwa naye, hakutaka kuwa na msichana mwingine, alimtaka Halima ambaye kwake alionekana kuwa mrembo kuliko msichana yeyote yule.

Walipanga kuonana majira ya saa kumi na moja jioni katika Hoteli ya Malovee iliyokuwa Sinza, lakini Wilbert alifika hapo mapema kabisa na kwenda katika mgahawa uliokuwa hotelini hapo.

Hakutaka kuonekana kuwa na presha, siku hiyo alitaka kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake. Akaagiza kinywaji na kuanza kunywa. Ilipofika saa 11:05, msichana huyo akafika mahali hapo huku akiendesha gari lake, akalipaki na kumfuata Wilbert pale alipokuwa.

“Nimechelewa sana?” Aliuliza Halima.

“Walaaa…mimi mwenyewe nimefika sasa hivi!” Alisema Wilbert, japokuwa alifika muda mrefu, lakini hakutaka kumfanya msichana huyo ahisi kama alichelewa sana.

Halima akakaa katika kiti kilichokuwa mahali hapo. Wilbert alibaki akimwangalia, japokuwa alimzoea sana Halima, lakini kila siku kwake alionekana kuwa msichana mpya kabisa. Hakutaka kukubali, siku hiyo alijiapiza kwamba ni lazima amwambie ukweli juu ya alivyokuwa akijisikia moyoni mwake kuliko kumuacha aondoke zake.

Wakanywa sana, baada ya hapo, Wilbert akaona kwamba huo ndiyo ulikuwa muda wenyewe, akaanza kumwambia kile kilichowafanya kuwa mahali hapo muda huo.

“Halima! Wewe ni msichana mrembo sana,” alisema Wilbert huku akimwangalia Halima.

“Najua! Wanaume wengi wameniambia hivyo ila najiona wa kawaida,” alisema Halima huku akiinama chini kwa aibu.

“Hakuna! U msichana mrembo mno. Ninakupenda kwa moyo wa dhati. Nimekuwa nikilificha hivi, lakini limekuwa likinitesa mno moyoni mwangu. Nimevumilia kwa kipindi kirefu, lakini nimekuwa kama mtu aliyekumbatia moto,” alisema Wilbert huku akimwangalia Halima machoni.

Alifunguka, hakutaka kumpa nafasi msichana huyo kujitetea kwa lolote lile. Alimwambia kuhusu hisia zake, jinsi alivyokuwa akiuendesha moyo wake kwa maumivu makali kila siku.

Halima hakujibu, alibaki kimya huku kila neno alilokuwa akiongea Wilbert likiingia moyoni mwake na kutulia kabisa. Baada ya kuzungumza kwa dakika arobaini na tano, Wilbert akaupeleka mkono wake katika mkono wa msichana huyo kuona kama angeweza kutulia, alipoushika mkono huo uliokuwa mezani, Halima akatulia.

“Ninakupenda Halima!” Alisema Wilbert, tayari kwa muda waliokuwa wameongea, kigiza kikaanza kuingia.

“Wilbert!”

“Naam Halima!”

“Najua unanipenda sana, ila….”

“Ila nini jamani?”

“Oopss…” Alishusha pumzi ndefu.

“Niambie tatizo nini!”

“Naogopa!”

“Unaogopa nini?” Aliuliza Wilbert.

“Basi tu, naogopa,” alisema Halima.

Hiyo ndiyo ilikuwa sababu yake, hakutaka kusema alichokuwa akikiogopa, lakini alimwambia ukweli kwamba huo haukuwa muda sahihi wa kuwa naye. Hilo lilimuumiza sana Wilbert, hakutegemea kama msichana huyo angeweza kusema maneno kama hayo.

Huo haukuwa mwisho, hata walipoachana, bado alimwambia Halima kuwa aliendelea kumpenda kwa moyo wa dhati na alikuwa tayari kufanya chochote kile kuhakikisha kwamba anakuwa wake.

Nyumbani, Halima alikuwa na mawazo tele, kila wakati alimfikiria Wilbert, ni kweli alimpenda, alitamani sana kuwa wake, lakini hali aliyokuwa nayo ndiyo iliyomfanya kumkatalia.

Je, nini kitaendelea? Tukutane Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Nyemo Chilongani | SIMU; +255 718 069 269

Leave A Reply