The House of Favourite Newspapers

Pesa Zaminya Demokrasia Uchaguzi 2020

0

KAMPENI za Uchaguzi Mkuu mwaka huu, zimeendelea kushika kasi, huku vyama vya siasa hususani vya upinzani, vikikabiliwa na ukata unaozuia vyama hivyo kushiriki kikamilifu tukio hilo la kidemokrasia nchini, IJUMAA wikienda linachambua.

 

Uchaguzi huo ambao ni wa sita tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, umetajwa kuwa uchaguzi wa kwanza kufanyika chini ya ukata, ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalazimika kutumia fedha kutoka hazina pekee.

 

Katika uchaguzi huo, NEC imetangaza kutumia bajeti ya Sh bilioni 331, fedha ambazo zinatoka Hazina, tofauti na chaguzi kuu nyingine.

 

Aidha, awali Machi mwaka huu, NEC iliomba kuidhinishiwa Sh bilioni 185.9 pekee, kabla ya kulazimisha kutumia Sh bilioni 331, ilhali bajeti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, NEC iliomba kiasi cha Sh bilioni 273.

 

VIONGOZI WALIA NJAA

Mmoja wa viongozi waliotia fora katika kusaka fedha kwa ajili ya kampeni, ni Mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu ambapo katika kila kampeni kabla ya kuanza kuhutubia, huwaomba wananchi waliohudhuria mikutano yake kuchangia chama hicho.

 

Pia Lissu huwaelekeza namna ya kutuma fedha hizo kwa njia ya simu za mkononi, kuelekea kwenye akaunti ya benki. Vivyo hivyo kwa upande wa mgombea urais wa Ada-Tadea, John Shibuda, naye alinukuliwa akieleza kuwa vyama ambavyo havipati ruzuku kutoka serikalini, ndivyo vinavyokabiliwa na ukata zaidi.

 

Alisema hatua hiyo imesababisha vyama hivyo kuchelewa kuanza kampeni, ilhali vyama vya CCM, Chadema na ACT Wazalendo, vikizidi kuchanja mbuga.

 

Wakati ratiba ya NEC ikionesha vyama vyote 15 vilivyosimamisha wagombea urais kutakiwa kuanza kampeni katika maeneo waliyopangiwa, hadi sasa baadhi ya vyama vimeshindwa kufi ka katika maeneo hayo kama vile Chauma, huku vyama vingine vikisita hata kuanza kampeni.

 

SABABU ZATAJWA

Baadhi ya wachambuzi waliozungumza na IJUMAA Wikienda, walifafanua kuwa, mojawapo ya mambo yaliyokwamisha upatikanaji wa fedha za kampeni, ni janga la maambukizi ya virusi vya Corona. Mmoja wa wachambuzi hao, Hamis Suleiman alisema janga hilo la Corona, limesababisha nchi wahisani kuacha kutoa michango yao kufanikisha uchaguzi huo.

 

“Angalia nchi kama Malawi ambayo imefanya uchaguzi katika kipindi ambacho Corona ilikuwa imechachamaa, ilifanya kwa shida sana kwa sababu hapakuwa na fedha kutoka nje, kwa hiyo na sisi hali ni hiyohiyo kwa sababu walitarajia kuwa tungeahirisha uchaguzi,” alisema.

 

Licha ya kwamba kufanya uchaguzi ni mojawapo ya njia ya kudumisha demokrasia, sasa wagombea wa nafasi mbalimbali kuanzia udiwani, ubunge na hata urais wa vyama mbalimbali, wanashindwa kushiriki uchaguzi huo kikamilifu kama njia mojawapo ya kidemokrasia.

 

Wagombea hao hususani wa vyama vya upinzani, wanakabiliwa na ukata hasa ikizingatiwa ni wafanyabiashara wachache wazawa walioweza kujitokeza kutoa michango yao, ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo hali ya uchumi wa mtu mmoja mmoja ilikuwa inatoa hamasa kwao kuchangia.

 

HAKUNA MBWEMBWE TENA

Licha ya kwamba katika chaguzi nyingi, ilizoeleka kukuta mabango ya wagombea urais kila kona ya nchi hususani wenye ushawishi mkubwa, hali sasa ni tofauti, kwani hakuna mabango wala ugawaji wa tisheti za bure.

 

“Kwa kweli hali ni mbaya, sisi mabalozi wa nyumba 10, tulizoea kuletewa marundo ya kanga, kofi a na tisheti za mgombea wetu wa urais, lakini sasa hali ni mbaya, kwani kila mtu anakwenda kujinunulia kwa wajasiriamali huko waliozitengeneza,” alisema mmoja wa mabalozi huko Mbagala.

 

Pamoja na hayo, vilevile magari ya matangazo yamepungua tofauti na chaguzi zilizopita, na haya yote yanasababishwa na ukata ambao wagombea wanashindwa kupambana nao.

 

Ikumbukwe kuwa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mchango wa Washirika wa Maendeleo kupitia mradi wa DEP, unaosimamiwa na UNDP, walitoa Sh bilioni 1.5 kugharamia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, ukarabati wa kituo cha kuchakata taarifa za wapigakura, uchapishaji wa maadili ya uchaguzi, maelekezo kwa watazamaji na mabango ya uhamasishaji wa uandikishaji kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Pia UNDP walitoa baadhi ya vifaa ambavyo ni pamoja na projekta saba kwa ajili ya mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi, kompyuta sita kwa Kituo cha Habari za Uchaguzi, kompyuta 171 na printa 171 kuwezesha mifumo iliyotumika katika kusajili wagombea, kituo cha kujumlisha na kutangaza matokeo katika halmashauri.

 

Vilevile waligharamia ununuzi wa vifaa na uanzishwaji wa Kituo cha Mawasiliano (Call Center) na Kituo cha Kusajili Watazamaji wa Uchaguzi.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply