The House of Favourite Newspapers

Peter Serukamba: Singida Tupo Tayari Kumpokea Rais Samia

0

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameelezea jinsi wananchi wa mkoa huo walivyojipanga kwa mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Singida, itakayoanza Oktoba 15, 2023.

Serukamba amesema wanatarajia kumpokea Rais Samia eneo la Sagala mpakani mwa Mkoa wa Manyara na Singida na kuelekea moja kwa moja kuzindua Shule ya Msingi Imbele ambapo itazinduliwa ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa shule zilizojengwa kupitia mradi wa Boost.

Amesema kwa upande wa elimu mwaka huu wa 2023, Rais Samia ametoa kiasi cha Tsh. Bilioni 9 ambazo zimetumika kujenga shule mpya 12, ukarabati wa madarasa, nyumba pamoja na ofisi za walimu.

Pia Rais Samia ametoa Tsh. bilioni 3 kwa ajili ya upanuzi wa shule za sekondari zinazochukua wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mbali na miradi hiyo ya elimu, pia kuna miradi mingi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Singida ambayo Rais Samia ataizindua ikiwemo mradi wa ujenzi wa Barabara ya Singida – Mbeya kipande cha km 56 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa vituo viwili vya polisi wilayani Ikungi na Mkalama, Ujenzi wa Daraja Wilayani Mkalama lililogharimu kiasi cha Bilioni 11, pamoja na kuzungumza na wananchi wa mkoa wa Singida katika mikutano ya hadhara.

Katika ziara hiyo ya Rais Samia inayoanza kesho, atafungua mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria katika eneo la Shelui wilayani Iramba huku akitarajiwa kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini mkoani Singida ambapo Mkoa wa Singida umepewa fedha takribani bilioni 71 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji vya Mkoa wa Singida ambapo Rc Serukamba amesema kufikia mwaka 2024 Kila kijiji katika Mkoa wa Singida kitakuwa kimepata umeme.

Leave A Reply