The House of Favourite Newspapers

PLO Lumumba Aukacha Ukurugenzi wa Kenya School of Law

0
Patrick Loch Otieno Lumumba.

MWANASHERIA maarufu nchini Kenya, Patrick Loch Otieno Lumumba, ajulikanaye kama PLO Lumumba, ameamua kutowania kipindi kingine akiwa Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya (Kenya School of Law – KSL) kwa vile anakwenda kufanya shughuli zingine.

“Niliiandikia bodi wiki iliyopita kuijulisha kwamba sitaongeza kipindi kingine na walikubaliana na ombi langu. Ninataka kuonyesha kwamba unaweza kutoa huduma na kuwaachia wengine fursa hiyo,” alisema Lumumba ambaye ameshika nafasi ya ukurugenzi wa shule hiyo kwa miaka mitatu. Vilevile, aliwahi kuwa mkurugenzi wa Tume Dhidi ya Rushwa ya Kenya kati ya mwaka 2010 na 2011.

PLO amepata umaarufu mkubwa kuhusiana na umakini katika kuzungumza kwake ambapo umahiri wake katika lugha ya Kiingereza umempatia heshima kubwa. Mwanasheria huyo alikuwa pia Mahakama Kuu akiiwakilisha Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), lakini juhudi zake hazikufua dafu kwani mahakama iliyafuta matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.

Chama cha Jubilee, National Super Alliance (NASA) na IEBC ambavyo Lumumba aliviwakilisha vinalazimika kukubaliana kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu. NASA imesema haitashiriki uchaguzi mwingine iwapo Mtendaji Mkuu wa IEBC hatang’olewa kwenye nafasi hiyo na wamepanga kufanya maandamano hadi jambo hilo litatuliwe.

Leave A Reply