The House of Favourite Newspapers

Polisi Ampiga Risasi Mkewe, Majirani Watano Kisha Naye Kujiua

0

TUKIO lisilo la kawaida limesababisha huzuni kutanda katika Mji wa Kabete nchini Kenya baada ya askari wa jeshi la polisi, kuwaua kwa kuwapiga risasi mkewe pamoja na majirani watano kisha naye kujipiga risasi iliyoyakatisha maisha yake, tukio lililotokea alfajiri ya Jumanne, Desemba 7, 2021.

 

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kabete, Francis Wahome amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililowaacha watu saba wakiwa wamefariki dunia, akiwemo askari huyo, mkewe, majirani pamoja na madereva bodaboda waliokuwa jirani na eneo la tukio.

 

Kamanda Wahome amesema tukio hilo limetokea majira ya asubuhi ya Jumanne katika eneo la makazi la J Apartments ambapo askari huyo aliyetambuliwa kwa jina la Konstebo Benson Imbatu, alikuwa akiishi na mkewe aliyefahamika kwa jina moja la Carol.

 

Taarifa zinaeleza kwamba majira ya kati ya saa 10 na saa 12 alfajiri, Jumanne Desemba 7, 2021, kulisikika mzozo kati ya wanandoa hao na muda mfupi baadaye, milio ya risasi ilisikika kabla ya askari huyo kutoka nje akiwa na bunduki aina ya AK 47 ambapo alianza kufyatua risasi hovyo akiwalenga majirani na madereva wawili wa bodaboda waliokuwa jirani na eneo hilo kisha na yeye kujipiga risasi kichwani.

 

Mashuhuda wa tukio hilo, wanaeleza kwamba baada ya kushtuliwa na milio mfululizo ya risasi, walipiga simu polisi ambapo walipowasili eneo la tukio, walikuwa watu saba wakiwa wamefariki dunia kwa kupigwa risasi, huku dereva bodaboda mmoja aliyekuwa amejeruhiwa vibaya, akikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta kwa matibabu.

 

Tukio hilo limeamsha hasira kwa wakazi wa eneo hilo ambao walianza kufanya fujo wakitaka hatua za haraka zichukuliwe, jambo lililolilazimu jeshi la polisi nchini humo kupeleka askari wengi eneo hilo kuzuia vurugu zilizokuwa zinaendelea.

 

Bado haijafahamika ni nini kilichosababisha askari huyo afanye tukio hilo na taarifa za kipolisi zinaeleza kwamba uchunguzi bado unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Leave A Reply