The House of Favourite Newspapers

Polisi apigwa mawe hadi kufa

MAOFISA wa polisi nchini Malawi wamemtaja ofisa aliyeuawa siku ya Jumanne wakati wa ghasia za maandamano dhidi ya serikali huko Msundwe – eneo la biashara magharibi mwa mji mkuu wa Lilongwe.

Msemaji wa polisi, James Kadadzerab, alikiambia kitengo cha habari cha AFP kwamba ofisa huyo aliyejulikana kama  Usumani Imedi, alipigwa mawe hadi kufa na waandamanaji na wahalifu.

Alikuwa ni  miongoni mwa maofisa waliowavamia waandamanaji ambao walikuwa wamefunga barabara katika eneo la Msundwe , eneo la upinzani, ili kuwazuia wafuasi wa Rais Peter Mutharika kuhudhuria mkutano wake wa kwanza wa kisiasa katika mji huo tangu ushindi wake wa uchaguzi uliokumbwa na utata mwezi Mei.

Wafuasi wa upinzani wamekasirishwa na jinsi tume ya uchaguzi ilivyosimamia uchaguzi huo, ikidai kwamba ulikumbwa na udanganyifu. Waziri wa Masuala ya Ndani, Nicholas Dausi, alisema kwamba watumiaji wengine wa barabara waliwataka maofisa wa polisi kuingilia kati baada ya waandamanji kufunga barabara hiyo inayotumika sana.

Wakati maofisa wa polisi walipowasili, walianza kuwapiga mawe kufikia kiwango cha kumpoteza afisa mmoja wa polisi. Maofisa wa polisi walirusha mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji lakini wakaendelea kujikusanya kabla ya kurusha mawe….na katika ghasia hizo walimkamata ofisa mmoja na kumpiga mawe hadi kufa, shahidi mmoja aliambia AFP.

Takriban watu 12 wamekamatwa na wengine wengi huenda wakakamatwa, kulingana na gazeti la Nation nchini humo.

Rais Mutharika baadaye alifanya mkutano katika mji mkuu na kuomba utulivu nchini humo, akisema: Hili ni taifa letu tusilichome.

Chanzo:Bbcswahili

Comments are closed.