The House of Favourite Newspapers

Prisons: Kichuya bora asicheze aisee

STORI: Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI | DAR ES SALAAM

MIKWARA mingine siyo poa kabisa kwani mabeki wa Prisons wakiongozwa na Salum Kimenya wamemuonya kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya bora akatae kucheza kwani wamepania kumkaba mwanzo mwisho.

Mabeki hao wa Prisons ambao timu yao ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza mzunguko uliopita kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wameapa kumzuia Kichuya kwa njia yoyote ili asifunge.

Leo, Prisons yenye pointi 29 katika nafasi ya sita inacheza na Simba yenye pointi 48 katika nafasi ya pili mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kimenya alisema wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanaifanya kazi yao vizuri katika mechi ya leo na hawatakuwa tayari kuona mchezaji yeyote wa Simba akiwasumbua hasa Kichuya.

“Nichukue nafasi hii kumtaka Kichuya hiyo kesho (leo) asiingie uwanjani kucheza kwani mabeki wote tumejipanga kuhakikisha hapati nafasi yoyote ya kuleta madhara langoni kwetu,” alisema Kimenya na kuongeza:

“Huu siyo utani, tumepanga kutofungwa kirahisi na hatutakuwa na mchezo na mchezaji yeyote hata Kichuya na kama akicheza ataona shughuli yetu.”

Hata hivyo, Kichuya ameliambia gazeti hili kwamba kutokana na kutofunga kwa muda mrefu atahakikisha anapambana katika mchezo wa leo ili afunge.

“Nitapambana katika mechi zote za Simba zilizo mbele yetu ili kuiweka timu yangu katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa pia nawania ufungaji bora,” alisema Kichuya mwenye mabao tisa akiongozwa na Simon Msuva wa Yanga mwenye mabao 10.

 

Comments are closed.