The House of Favourite Newspapers

Mabao 26 ya Yanga yawatisha Ngaya

STORI: Elie Djouma | CHAMPIONI | COMORO

KWA rekodi Yanga imecheza na timu mbili za Comoro hadi sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kuzifunga jumla ya mabao 26 katika mechi mbili za nyumbani na ugenini.

Rekodi hiyo imewatisha wachezaji wa Ngaya Club de Mbe ambao kesho watacheza na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Moroni jijini Moroni.

Hii ni mara ya tatu kwa Yanga kucheza na timu ya Comoro, kwani mwaka 2009 ilicheza na Etoile d’or de Mirontsy na kuifunga jumla ya mabao 14-1 (8-1 na 6-0), mwaka 2014 ikaitoa Komorozine kwa mabao 12-2 (7-0 na 5-2). Jumla Yanga ilifunga mabao 26 na kufungwa matatu.

Nahodha na beki wa kutumainiwa wa Ngaya, Said Hachim alisema; “Wenzetu walifungwa idadi kubwa ya mabao, hiyo ni rekodi inayoonyesha tunakutana na timu yenye uzoefu mkubwa.

“Jukumu letu kwanza ni kuheshimu rekodi hiyo halafu tujipange kujua tunazuia vipi nasi tusikumbane na kilichowakuta wenzetu, Mungu atatusaidia na tutapambana.”

Ngaya Club inapatikana katika mji mdogo wa Mde Bambao unaopatikana mita 400 kutoka kusini mwa mji mkuu wa Comoro, Moroni.

Comoro ni nchi inayoundwa na visiwa vinne ambavyo ni Ngazija, Anjuani, Moheli na Mayotte. Kila kisiwa hucheza ligi yake kisha mabingwa wanakutana kucheza ligi ya kupata bingwa wa Comoro katika Ligi Kuu na Kombe la Ligi.

Baada ya mechi ya kesho Jumapili, timu hizo zitarudiana Jumamosi ijayo ya Februari 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Comments are closed.