The House of Favourite Newspapers

Prof. Jay Huzuni Kila Kona, Mashabiki Zake Waongea na Gazeti la Ijumaa

0
Msanii nguli Bongo, Joseph Haule ‘Prof Jay’.

MGOGORO wa kiafya wa msanii nguli Bongo, Joseph Haule ‘Prof Jay’ umemtenga na jamii kwa takriban mwaka mzima na kuacha huzuni kila kona kutoka kwa mashabiki zake.

Chachu ya masikitiko katika mioyo ya watu juu ya afya ya msanii huyo imeibuka baada ya wiki iliyopita gazeti hili kuchapisha makala iliyolenga kuhamasisha wasanii wenzake kuungana naye katika kipindi hiki kigumu.

“Mwandishi ni kama umetonesha kidonda changu kwa Pro. Jay, sijui yuko katika hali gani?” Juma Hussein wa Kisarawe, mkoa wa Pwani alituma ujumbe wake kwenye Gazeti la Ijumaa.

Tangu Januari 2022, Prof. Jay aripotiwe kuugua na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ‘ICU’ katika hospitali ya Taifa Muhimbili hajaonekana uraiani wala kujihusisha na siasa au sanaa kwa namna yoyote.

Ukimya wa hali ya msanii huyo na wasanii wenzake katika kuzungumzia hali ya Prof Jay, ndiyo uliomsukuma mwandishi kuwahoji wasanii wenzake wamemtenga kama alivyoimba mwenyewe kwenye wimbo wake wa

MSINITENGE.

“Unaposikia mashairi kama haya, lazima moyo utauma, utajiuliza ni wangapi miongoni mwa rafiki zake Prof. Jay wamemtenga katika kipindi hiki kigumu anachopitia? Ni wasanii wangapi aliowatoa kimuziki wanaungana naye na familia yake katika siku hizi za giza?

Mbona hatuoni michango ya wasanii wenzake katika kumuwezesha kupata maziwa, hakuna hata shoo za kuchangisha fedha kuisaidia familia yake kumuuguza, vipi tayari amesahaulika?

Ina maana mapema hivi wasanii wa Bongo Fleva wakubwa na wadogo kimuziki wamesahau kuwa Prof Jay ni miongoni mwa wachonga barabara ya muziki nchini wanayoipita wengi hivi sasa na kuvuna mamilioni?” Hii ni sehemu ya makala ya makala ya mwandishi wetu iliyochapishwa katika Gazeti laIjumaa toleo lililopita kwenye ukurasa wake wa kumi na tano.

Tangu makala hiyo itoke, chumba cha habari na mwandishi husika wamekuwa bize kupoke ujumbe na simu zenye masikitiko juu ya changamoto anazopitia Prof. Jay pamoja na familia yake akiwemo mkewe.

Wadau na mashabiki wa nguli huyo wa sanaa ya muziki wa kizazi kipya aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Mikumi kupitia chama cha Chadema wamekuwa wakirusha lawama, maombi na hamasa kwa wenzao kuhakikisha Prof. Jay hatengwi kwenye kipindi hiki cha giza cha maisha yake.

 

“Umendika makala nzuri, inachoma moyo, lakini hukueleza tunawezaje kutoa mchango wetu kwa Prof. Jay ili kuonesha tuko pamoja naye,” Husna Shabaki wa Mwanza alituma ujumbe kwa njia ya simu kwenye maneno hayo. wHata, hivyo mwandishi wa makala ya wiki iliyopita iliyokuwa na kichwa cha habari.

“MASIKINI PROF. JAY alikana kuandika makala iliyolenga kuhamasisha watu watoe michango kwa ajili ya kusaidia mapambano juu ya afya ya msanii huyo. “Sikutaka hilo, nilikuwa nawakumbusha wasanii wenzake, wasimtenge, mashabiki zake wasimsau mapema, kwa sababu bado yupo duniani.

“Tamaa yangu ni kuwafanya watu kuonesha upendo na kujitolea kwa watu kabla hawajafa. “Nimeshukuru kupokea shukrani na pongezi kutoka sehemu mablimbali za nchi yetu, hii imenipa hakika niliyoiamini kuwa Prof. Jay ni kipenzi cha wadau wengi wa muziki,” alisema mwandishi wa makala ya wiki iliyopita.

Aliongeza kuwa, kazi ya kuwambusha watu kujaliana katika shida ni ngumu na kuongeza kuwa amewahi kulalamikiwa pale alipokuwa akiwahamasisha watu kumuombea msanii wa Kundi la Ze Original Comedy, Joseph Shamba a.k.a ‘Vengu.’ “Ilifikika hatua nikaambiwa mimi na bosi wangu aliyeniajiri tunatumia ugonjwa wa Vengu kuuza magezeti jambo ambalo halikuwa sahihi.

“Leo tunapozungumza kuhusu Vengu ni zaidi ya miaka kumi imepita hakuna anayejua hali yake, amesahaulika kama mfu na wale waliokuwa wasanii wenzake wanaendelea na maisha yao kama kawaida.

“Enzi hiyo ya Ze Comedy ilikuwa balaa, Vengu alifanya kazi kubwa lakini amesahaulika, ndivyo Wabongo walivyo, naliona hili likitokea kwa Prof Jay.

“Ndiyo maana nawaambia wadau hatutakiwi kumtenga kwa sababu ni msanii mwenzetu, mdau wa muziki na Mtanzania mwenzetu,” alisema mwandishi huyo. Wakati hayo yakijitokeza, familia ya Pro.Jay haijaomba msaada wowote wa kukabiliana na hali ya ndugu yao lakini ukweli ni kwamba serikali iligharamia matibabu ya msanii huyo alipolazwa hospitalini.

Taarifa kupitia simu na meseji ambazo Ijumaa imezipokea kutoka sehemu mbalimbali ya nchi zinaonesha kuwemo wa watu ambao wanataka kutoa michango yao ili kuonesha mahaba yao kwa msanii huyo ambaye ni miongoni mwa walioifanya sanaa ya muziki wa kizazi kipya iheshimike.

Kwa mujibu wa habari kutoka chanzo cha karibu zinadai Prof Jay bado anaendelea kupigania afya yake ingawa nafuu ya ‘Kiswahili’ amepata. Kituo kimoja cha Runinga nchini imemkariri mkewe akisema.

“Akipona kabisa anataka kuja kurudisha shukrani zake kwa Mungu, kwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwenye hospitali zote alizopita, Kwa Watanzania pamoja na viongozi wote wa dini, na mashabiki zake, anataka aje azungumza kwa kirefu,” alisema mke huyo ingawa jambo hilo halijatimizwa.

Kama una maoni kuhusu habari hii unaweza kuwasiliana nasi kupitia namba 0714 895 555.

Leave A Reply