The House of Favourite Newspapers

Prof. Kamuzora Asisitiza Uhifadhi wa Mazingira Nchini

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Prof. Faustin Kamuzora (kulia) akiwa na mkurugenzi anayeshughulika na mazingira, Richard Munyungi.

KATIKA kuelekea siku  ya  Mazingira Barani Afrika inayotarajiwa kuadhimishwa Machi 3, Mwaka huu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Prof. Faustin Kamuzora amesema kuwa Watanzania wanapaswa kulinda na kuhifadhi mazingira yanayowazunguka ili kuondokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kujitokeza.

Mkutano na wanahabari ukiendelea

Kauli hiyo ameitoa leo wakati alipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo alisema Machi 3 ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine za Afrika katika kuadhimisha siku ya mazingira Afrika.

“Siku hii imetengwa kwa lengo la kila mwaka kukumbuka umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira Barani afrika.

“Azimio la kuadhimisha siku hii lilipitishwa na kuamuliwa na Baraza la Mawaziri wa Mazingira wa nchi za afrika kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika Kusini mwaka 2002,” alisema.

Alifafanua  kuwa siku hiyo iliamuliwa iwe kielelezo cha kukuza weledi kuhusu kupambana na uharibifu wa mazingira  na kuenea kwa hali ya jangwa katika Bara la Afrika.

Aliongeza kwamba  kwa kutambua juhudi na kazi iliyofanywa na marehemu Prof. Wangari Maathai, aliyefariki Septemba 25, 2011,  na mchango wake katika hifadhi ya mazingira na kuwezesha wanawake katika usimamizi endelevu wa maliasili na mazingira kwa ujumla, Umoja wa Afrika uliamua tarehe hiyo uwe siku ya maadhimisho hayo kila mwaka na  iwe pia ni siku ya kumbukumbu yake.

NA DENIS MTIMA/GPL

Comments are closed.