The House of Favourite Newspapers

Prof. Ndalichako Anaficha Udhaifu Bodi ya Mikopo?

0

 

“TAMKO lao halina adabu, kama wanataka kutikisa kiberiti, nawaambia kiberiti kimejaa njiti,” hiyo ni kauli ya kibabe ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako aliyoitoa dhidi ya uongozi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso).

 

Pia Prof. Ndalichako aliuagiza uongozi wa chuo hicho kikuu, kuwachukulia hatua ndani ya saa 24 uongozi wa wanafunzi hao, kwa sababu tu walitoa saa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kushughulikia changamoto zao.

 

Bila ajizi, uongozi wa chuo nao ukachukua hatua ya kuwasimamisha wanafunzi sita wa chuo hicho ikiwamo viongozi wa Daruso.

 

Hakika adhabu iliyochukuliwa dhidi ya wanafunzi, ni mojawapo ya adhabu za kukurupuka, ni adhabu iliyotokana na shinikizo la waziri bila kutazama kiini cha tatizo.

 

Yamkini angefuatilia kiini cha tatizo asingetoka hadharani na kauli za kibabe namna ile kama vile anapambana na chama cha siasa cha upinzani.

 

Nasema hivyo kwa sababu hoja wa wanafunzi hao ni hoja za msingi, ambazo zingepaswa kutatuliwa kwa wakati na kama kungelikuwa na ucheleweshwaji wowote basi bodi ya mikopo ingelipaswa kutoa ufafanuzi wenye kuridhisha badala ya kuwapiga kalenda kila wanapofuatilia fedha zao.

 

Hoja za wanafunzi hao ni kwamba wapo wanafunzi wanaoendelea na masomo waliokatwa fedha zao, wapo wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopitishwa kupata mikopo lakini mpaka sasa hawajapata, vilevile wa mwaka wa kwanza wenye sifa za kupata mkopo ila wamenyimwa licha ya kukata rufaa.

 

Ni hoja ambazo bodi ya mikopo ingelipaswa kukaa na wanafunzi hao kutatua kadhia hiyo kwa sababu wanafunzi hao walifungua chuo tangu Novemba 4 mwaka huu, wakafuatilia madai yao zaidi ya wiki sita lakini mpaka wanatoa tamko hilo tayari walipigwa kalenda mara kadhaa.

 

Lakini jambo la kushangaza waziri ametumia mamlaka yake kuwashughulikia wanafunzi hao waliokuwa wanapigania haki zao na za wenzao, ili wapate kuanza mitihani kwa amani kama walivyoeleza kuwa wiki ijayo wanatarajia kuanza mitihani.

 

Inasikitisha kuona waziri ambaye ni mwanamama anakosa busara kama mzazi, bila kujali kuwa wapo wanafunzi waliotoka katika familia masikini, wanafunzi wasiokuwa na ndugu kabisa hapa jijini Dar es Salaam ili wawasitiri wakati wakisubiri danadana za bodi ya mikopo.

 

Badala yake anatoa vitisho, na kuagiza kuwa washughulikiwe, ilihali anafahamu kabisa kuwa ucheleweshwaji huo wa fedha zao kutoka bodi ya mikopo kunatokana na urasimu uliomo ndani ya bodi hiyo na serikali kwa ujumla.

 

Hili suala ni sawa na kufunika kombe mwanaharamu apite, haiwezekani, kutoa vitisho na kuchukua hatua kwa wanafunzi wanaodai haki zao, bila kuwachukulia hatua bodi ya mikopo, hii ni sawa na kuficha maovu ya utendaji hafifu wa bodi ya mikopo.

 

Nasema hivyo kwa sababu ni wanafunzi wengi waliokosa mikopo, ikumbukwe kuwa bodi ya mikopo ilisema imepokea jumla ya maombi 87,747 ambapo kati ya maombi hayo, ni maombi 82,043 sawa na asilimia 93.4 yalikuwa yamekidhi vigezo vya maombi na mwaka jana yalikuwa maombi 81,425 yaliyokidhi.

 

Lakini mpaka Disemba mwaka huu ni wanafunzi 49,485 pekee waliopewa mikopo, na ndani yao wamo hao ambao wameidhinishwa kupewa lakini wanapigwa kalenda na wakidai wanasimamishwa masomo.

 

Jambo lingine linalotia shaka utendaji wa bodi ya mikopo ni kuficha orodha halisi ya wanafunzi waliokata rufaa, kwa sababu haikutaja idadi ya wanafunzi waliokata rufaa bali walioshinda ambao ni 600 pekee ikilinganishwa na mwaka jana ambao walikuwa 2,000.

 

Hii ina maana kuwa kwa mwaka huu hao wanafunzi zaidi ya 32,000 waliokosa mikopo licha ya bodi kusema wanavigezo, vilevile walikata rufaa.

 

Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Bunge limeidhinisha Sh bilioni 450 kugharamia mikopo ya wanafunzi elmu ya juu, hadi Disemba mwaka huu zimetolewa bilioni 202 sawa na asilimia 45 pekee, ilihali mwaka wa fedha unatarajia kuisha kuanzia Juni mwakani.

 

Yamkini hiyo asilimia 55 ingelikuwa imetolewa japo kidogo kwa wakati kusingekuwepo na rabsha hizi zinazojitokeza sasa.

 

Tunafahamu kuwa waziri anapigania tonge lake, ili Rais asimwone ameshindwa kutatua changamoto za sekta ya elimu nchini, lakini utatuzi wa changamoto hizo unahitaji busara na si ubabe kama huu alioudhihirisha.

Leave A Reply