Promota Semunyu: Selemani Kidunda Dhidi ya Tshimanga Katompa Rasmi Julai 30 Songea
PROMOTA wa mapambano kutoka Kampuni ya Peak Time Media (PTM), Meja Seleman Semunyu ameweka wazi rasmi kuwa pambano la kisasi kati ya Mtanzania, Selemani Kidunda dhidi ya Mkongomani Tshimanga Katompa linatarajiwa kupigwa Julai 30, mwaka huu Songea mkoani Rukwa.
Pambano hilo litakuwa la pili kwa mabondia hao kukutana ambapo mwezi Desemba mwaka jana walipambana jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya TKO, kufuatia Kidunda kupata jeraha la kupasuka usoni.
Semunyu aliyasema hayo katika iftar maalum iliyoandaliwa na Peak time Media kwa wadau mbalimbali wa mchezo wa ngumi, iliyofanyika juzi Alhamisi jijini Dar es Salaam.
Meja Semunyu alisema: “Baada ya kuwepo kwa mahitaji ya wadau wengi wa ngumi juu ya kutaka kujua nani mbabe kati ya Kidunda na Katompa sisi tumewasikia na sasa tunawatangazia rasmi kuwa pambano hilo la kisasi litapigwa Julai 30, mwaka huu, Songea mkoani Rukwa hivyo tunaomba sapoti yenu.”