The House of Favourite Newspapers

RAHA YA MUME ASIKUPE TABU SANA!

JUMATANO nyingine hiyo tumekutana shoga yangu! Anti Naa wa kujimwayamwaya nipo tena mjengoni shoga! Heee heeeiyaaa na watanawa maji ya visima mwaka huu, ndo hivyo tena lao jembe wangu mpini, upo?

Shoga najua maneno yangu kama maji vile, ukiwa na kiu utayanywa, ukiwa na njaa lazima utakula tu! Tena waambie wasinichoshe miye, mdogo wangu pesa siku hizi, nikiongea ndiyo nakufunda hivyoooo!

Leo sitaki kumchamba mtu hapa! Maana utawasikia loo Anti Naa kila siku wanawake, kwani miye mwanaume? Shoga leo nipo na kina baba wale wavivu majumbani, wao wakishaoa basi wanajua mwanamke ndiyo hausigeli, ndiyo hausiboi!

Hakuna kitu kinachokera kama kuishi na mwanaume asiyejua hata kuosha vyombo! Shuuuutuuuuu! Mwanaume lazima ujue kupika bwana! Kwanza hii itakupunguzia utegemezi na kukufanya uonekane hujaoa mpishi bali msaidizi na ukiwa kwenye ndoa basi mara mojamoja kumpikia mkeo na watoto, au siyo shoga?

Mwanaume lazima ujue kufua siyo mkeo unaishi naye aumwe au asafiri ulundike minguo mwezi mzima kisha unasubiria wa kukufulia, matokeo yake unajikuta unavaa nguo kwa kurudia bila kufua, heee heeeiyaaaa! Mwanaume lazima ujue kufanya usafi wa ndani, kudeki na kupangilia mpangilio wa vitu ndani, lazima pia ujue kuosha vyombo vya kupikia!

Shoga mwanaume lazima uhakikishe unapokuwa faragha na mwezi wako usimuache bila kumridhisha, siyo unavyoridhika wewe basi imetoka, unamuacha anakuitaji zaidi matokeo yake anaishia kuvumilia moyoni tu au kuchepuka! Wengine wanashindwa kujua kama mwanaume lazima umpende mwanamke wako kama unavyompenda mama yako naye atakujali kama vile atakavyomjali mtoto wake, upo?

Mwanaume lazima uwe mwenye elimu. Siyo elimu ya darasani, hata elimu dunia, elimu ya mwanaume lazima imsaidie kulitazama tatizo na kulifanya liwe dogo kisha alitafutie ufumbuzi au nadanganya shogaaaaa?

Kama ulikuwa hujui, mwanaume lazima uwe msafi wa kimwili, utoe pumzi safi kinywani, siyo kukimbilia dawa za mswaki hata miti shamba inahu! Ukiongea uwe na pumzi nzuri, uwe nadhifu kimavazi hata kama huna mavazi mengi, lazima uwe maridadi kwa mavazi uliyonayo.

Mwanaume lazima uwe na misimamo, usiwe mtu wa kuyumbishwa na kuwa kama bendera fuata upepo. Unapokuwa upo sahihi simamia msimamo wako na kama hauko sahihi kubali kujifunza. Uwe mfurahishaji machoni mwa watu, siyo wewe unakuwa mkoloni tuu hata kwa watoto wako? Mkeo? Hapana lazima uwe kiungo muhimu cha furaha kiasi kwamba ukikosekana basi unamisiwa na siyo watu kufurahia kukosekana kwako.

Najua utakuwa unajiuliza leo Anti Naaa ameguswa na nini, siyo msiba huu useme utaanua matanga! Nataka kukwambia wewe mwanaume na wewe mwanamke mtambuane!

Kuna wanaume hawajitambui katika maisha wao bora siku iende! Mwanaume lazima ujiamini na kile ukifanyacho. Lazima uwe tayari kutoa msaada kwa mtu iwe wa kimali au kihali. Bila kujalisha uchumi wako ni lazima uhakikishe familia yako inapata mahitaji makubwa ya msingi ambayo ni chakula, mavazi, malazi na elimu.

Kwa kumalizia, mwanaume lazima uamini yajayo yanafurahisha! Hii bila kujalisha changamoto unazopitia lazima uwe na moyo wenye tumaini, kumbuka kunyong’onyea kwako kunamfanya mwanao au mkeo au wazazi au jamii kwa ujumla wajihisi wenye unyonge zaidi. Kwa leo nifumbe domo langu! Ni mimi Anti Naa, Shangingi Mstaafu!

Comments are closed.