The House of Favourite Newspapers

Rais Dk. Samia Atuma Salamu Kwenye Tamasha La Tuzo Za Filamu 2023, Awashushia Neema Bongo Muvi

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam, 16 Desemba 2023: Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameipongeza Bodi ya Filamu nchini chini ya Katibu wake Mtendaji Dk. Kiagho Kilonzo kwa maboresho makubwa ya tuzo hizo mwaka huu hali iliyomfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kutuma salamu kwenye tamasha hilo na kushusha neema kwenye tasnia hiyo.

Nape ambaye alimuwakilisha Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo Dk. Damas Ndumbaro, akizungumza kwenye hafla hiyo amesema ameagizwa na Rais, Dk. Samia awafikishie salamu wanatasnia hiyo kuwa pamoja na ule mfuko aliouanzisha amesema yuko tayari kuongeza fungu la Mama.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dk. Kiagho Kilonzo.

Amesema kwasababu Mama ameona chachu ya nguvu iliyowekwa na kuibua mafanikio hayo, Waziri Nape amesema yuko kwenye tamasha hilo kwa niaba ya serikali hivyo basi anawathibitishia kuwa serikali ya awamu ya sita inathamini kazi sanaa ya filamu.

Nape amesema ndiyo maana Rais Samia mwenyewe akaamua kuwa sehemu ya wasanii kwasababu anaitambua kazi sanaa ya filamu na kazi aliyoifanya imetuletea fedha nyingi na heshima kubwa duniani. Aliendelea kusema Nape;

“Jioni ya leo nimekuja kuwathibitishia kuwa serikali anayoiongoza ipo pamoja na nyie, itawaunga mkono, haitawatupa na tutafanya mambo mawili makubwa, moja ni tutaendelea kuboresha sheria kanuni na katiba ili kulinda kazi zenu zisipotee na la pili tutahakikisha kila uwezo unapopatikana tunawekeza kuhakikisha tunapata mtaji wa kuboresha kazi zenu.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akifikisha salamu za Rais Dk Samia Suluhu.

“Rais Samia anaamini katika tasnia ya filamu Tanzania inaweza kuwa ya kwanza kwasababu vipaji vipo kwa kutosha mnachohitaji ni kushikwa mkono na kujengewa mazingira bora ambayo Rais Samia yuko tayari kuyafanya na yeye mwenyewe ipo siku atakuja kuwatembelea.

“Kwahiyo jioni ya leo katika salam zake anawapongeza wale wote waliofanya vizuri lakini anawataka mtumie nafasi hii kujipanga vizuri ili tuzo zijazo mfanye vizuri zaidi. “Lakini ndugu zangu la mwisho ukiangalia takwimu kwanza fedha ambazo Rais alizitoa kwenye mfuko ambazo zimeenda kwa wasanii ni karibu milioni mbili nukta tisa na tunaona matokeo yake.

“Lakini katika tasnia zinazokuwa kwa kasi tasnia ya filamu inakuwa kwa kiasi kubwa awali iliyumba kipindi cha Uviko lakini takwimu zinaonesha mmeanza kwenye kurudi vizuri tena kwa kasi mno.

“Nataka kutoa wito kama Waziri ambaye nasimamia Habari, Mawasiliano na Tehama, wengi wenu nawaona wako kwenye mitandao na wana wafuasi wengi kwahiyo mnainfluency ya watu wengi wanawafuatilia.

“Sasa twendeni tukawe mifano mizuri kwa wale wanaotutazama ili wakitutazama watamani kuwa kama sisi kwa mifano mizuri tunayowaonesha.

“Wasanii wa filamu wawe kipaumbele kwa mifano mizuri tunayoionesha, naomba nimalizie kwa kusema wasanii wa filamu tumuunge mkono, tumsaidie, tumuombee, Mama yetu kwani anatupeleka safari njema na tutafika salama tumuombee na sisi vijana wake tuko tayari kusonga naye mbele.

“Mwisho niwatakie kila la kheri tunapomalizia tuzo zetu za mwisho na niwatakie krismasi njema na wote tuvuke na tusonge mbele mwaka mpya 2024. Asanteni kwa kunisikiliza. HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GLOBAL PUBLISHERS                

Leave A Reply