The House of Favourite Newspapers

Unataka kuanzisha biashara mpya? Chunga mambo haya

Jarida la Bloomberg la Marekani limeeleza kuwa, takriban bi­ashara nane kati ya kumi ambazo huanzishwa, hufa baada ya muda wa miezi 18 (mwaka mmoja na nusu). Takwimu hizi zinamaanisha kuwa katika kila watu kumi ambao wanaanzisha bi­ashara mpya, nane kati yao biashara zao hazitakuwepo baada ya miezi 18.

 

Hii inaonesha kuwa kuna umuhimu wa kujipanga na kujiandaa kama unapanga kuanzisha biashara ili usiwe mmoja wa wale ambao bi­ashara zao hazitafanikiwa. Ili kujiepusha kuwa kati ya watu ambao biashara zao zinafeli na hazifiki mbali, ni muhimu kujifunza sababu ambazo hu­wafanya wengi waishie njiani na washindwe kufanikiwa;

 

MOJA

Moja ya mambo yanayofanya biashara zife ni kukosekana kwa utatifi kabla ya kuanzishwa kwake. Wengi huanzisha biashara bila kujipa muda wa kutosha kuchunguza aina ya biashara wanazotaka kufanya na kujua kama ni biashara au la. Kosa mojawapo katika hatua hii ambalo wengi huwa wanalifan­ya ni kuangalia faida tu inayowe­za kupatikana na kusahau kuwa kuna mambo mengine mengi sana yanapaswa kuzingatiwa.

 

Moja ya vitu ambavyo unatakiwa kuvifanyia utafiti ni mwendelezo wa biashara unayotaka kuifanya. Kuna watu wengi wanaparamia biashara za msimu na kuingiza pesa nyingi bila kujua kuwa wakati wanaingia kumbe ndiyo msimu wa mafanikio wa biashara hiyo ulikuwa unaishia.

Ni kama vile kuanza kuagiza miamvuli makontena 100 wakati kumbe kipindi cha mvua kinaishia. Si unakumbu­ka watu walivyovamia mayai ya kwale? Leo yako wapi. Ni muhimu kuangalia asili ya biashara na kujua itadumu muda gani.

Pia ni muhimu sana ku­fanya utafiti wa upatikanaji wa bidhaa hasa kama unafanya biashara ambayo inahitaji malighafi. Kuna mtu niliwahi kukutana naye ambaye baada ya kusikia biashara fulani inalipa, akaenda kununua mashine nyingi sana kwa pesa kubwa, lakini baada ya muda akakosa kabisa kupata ma­lighafi na akasitisha uzalishaji hadi leo. Na wewe jiulize, hivi bidhaa hizi ninazoanza kuuza au kuzalisha nina uhakika wa kuzipata kila nitakapohitaji?

 

Haya ni baadhi ya mambo ya kuangalia hata kabla hujaangalia kiwango cha mtaji ambacho unahitaji. Usipara­mie biashara bila kufanya utafiti na kama unaona huwezi kufanya utafiti mwenyewe, unaweza kutafuta watu ambao wanaweza kukusaidia kitalaam zaidi.

 

MBILI

Jambo lingine linalofanya bi­ashara zikwame ni kutojiamini katika bidhaa unazouza au huduma unayotoa. Changa­moto mojawapo wanayopata watu wanaoanzisha biashara ni kuamini kuwa wanatakiwa waonewe huruma na watu watumie bidhaa zao kama njia ya kuwasapoti.

Hili ni kosa kubwa sana, unapoingiza sokoni bidhaa au huduma yoyote ile, una­takiwa uingie kwa kujiamini na uoneshe ubora na thamani ya kile unachokifanya bila woga.

 

Watu wengi wameingia kwenye biashara na kwa saba­bu ya kutokujiamini wameji­wekea thamani ndogo sana kuliko hata ile ambayo wa­nayo (undervaluing) matokeo yake wamejikuta wanabakia chini na watu wanawachukulia kama watu ambao hawana thamani na wanashindwa hata kuongeza bei ya bidhaa zao wanazotoa.

 

Unapoamua kuwa mfanya­biashara kumbuka kuwa watu wanataka kuona kujiamini kwako katika biashara unayofanya na kumbuka kuwa wakiona mfanyabiashara yeyote hajiamini, basi na wao pia wataacha kuamini kwa kiwango kikubwa bidhaa au huduma unayotoa. Je, una­jiamini?

TATU

Kitu kingine kinachoua biashara nyingi ni wafanya­biashara kushindwa kujua wateja wao. Moja ya vitu ambavyo vinaweza kuku­potezea muda na fedha katika kukuza biashara yako ni pale unapojaribu kuwauzia watu ambao siyo sahihi. Kumbuka kutangaza biashara yako kwa bidii na kwa gharama kubwa haitakupeleka unakotaka. Ni lazima uhakikishe kuwa un­auza biashara yako kwa watu sahihi.

 

Hebu jiulize, umeshawahi kuona tangazo lolote la soda lenye wazee? Matangazo yao yote wamejaza vijana, kwa nini? Wazee wengi wako makini na vyakula hasa vyenye sukari na kampuni za soda wanajua kabisa hawa siyo wateja wao wa kudumu. Wateja wao wengi ni vijana na ili kuwapata vijana wengi ina­walazimu kutumia vijana zaidi kufanya matangazo yao.

 

Leo, jiulize hivi biashara yangu hii nawalenga watu wa namna gani? Inawezekana ukawalenga watu kutokana na umri wao, kutokana na jinsia zao au hata kutokana na kiwango chao cha kipato.

Kitu muhimu sana kwenye kukuza biashara yako ni kuhakikisha kuwa lile kundi ambalo unalilenga unalifikia mara kwa mara bila kuchoka. Usipoteze nguvu kubwa katika kujaribu kuwafikiwa watu am­bao siyo kundi la wateja wako.

Kumbuka kuwa mikakati yako yote inatakiwa ilenge ku­wafikia kundi la watu ambao ndiyo hasa wateja wako.

Comments are closed.