The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli gumzo mitandaoni, Wakenya wasifia uchapakazi wake

john-magufuli-presidential-inaugurationRais JohnPombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

SIFA kubwa aliyonayo Rais Dk John Pombe Magufuli ya uchapakazi na kufuatilia kwa karibu shughuli za serikali imekua gumzo mitandaoni huku akipongezwa kwa utendaji kazi wake kwani ni ujumbe tosha, si kwa maofisa wa Tanzania pekee, bali na nchi za jirani pia, kuwaacha viongozi wa nchi hizo kwenye wakati mgumu.

Kenya ambayo imekuwa ikifuatilia siasa za Tanzania tangu wakati wa kampeni, imeonesha kupenda mbinu za utendaji kazi wa Magufuli na wananchi wake wanatamani mtu kama yeye.

Kwa kipindi kifupi alichoingia madarakani, Magufuli amefanya mambo makubwa na wananchi wamependa.

Ziara yake ya kushtukiza kwenye Wizara ya Fedha, Hospitali ya Taifa Muhimbili kufichua uovu mwingi na kupelekea kufutwa kwa bodi ya wakurugenzi wa hospitali hiyo na kumuondoa Kaimu Mkurugenzi wake, Dk Hussein Kidanto.

Ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za serikali kwaajili ya kugharamia safari za nje za viongozi wa nchi, Magufuli aliamua kuzisitisha mara moja.

Dk Magufuli pia alielekeza kiasi cha shilingi mil. 225 zilichangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge kupongezana mjini Dodoma zipelekwe kwenda kununua vitanda kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili. Badala yake shilingi milioni 15 pekee zilitumika kwaajili ya sherehe hiyo.

Siku chache baadaye vitanda hivyo na vifaa vingine vilinunuliwa na kupelekwa Muhimbili.

Jumatatu hii (jana) Magufuli alitangaza kuondoa sherehe za maadhimisho ya siku ya Uhuru December 9 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maandalizi hayo zitumike kwa mambo mengine muhimu.

Hayo na mambo mengine yamefanya Dk Magufuli atrend nchini Kenya.

Comments are closed.