The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli Kuhamia Dodoma 2018, Samia Mwaka Huu

Rais Magufuli akisalimiana na Makamu wake, Samia Suluhu, kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

WAKATI wowote mwaka 2018 Rais John Magufuli atahamia makao Makuu ya Nchi, Mjini Dodoma na si mwaka 2020 kama ilivyotangazwa awali huku Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuhamia Dodoma mwishoni mwa mwaka huu kwa kuwa maandalizi yapo tayari.

 

Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Alhamisi  Desemba 7, 2017 wakati wa uzinduzi wa ofisi za Umoja wa Mataifa Dodoma ambapo amesema hadi sasa watumishi 2,346 kutoka wizara zote wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wameshahamia Dodoma.

 

Jana Jumatano Desemba 6, 2017, Majaliwa alikagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais eneo la Kilimani Mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi ya mkuu wa mkoa huo.

 

Magufuli alitangaza kuhamia Dodoma  katika sikukuu za mashujaa zilizofanyika kitaifa kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 2016 tangu nchi ipate uhuru ambapo uamuzi huo ulipokewa na Waziri Mkuu Majaliwa aliyetangaza ratiba ya uhamiaji wa Serikali katika kipindi cha miaka mitano baada ya yeye mwenyewe kuhamia Septemba Mosi, 2016.

 

Kwa mujibu wa Majaliwa, ratiba ya Serikali kuhamia Dodoma ilianza Septemba 2016 hadi 2020.

Awamu ya kwanza iliyomhusisha yeye mwenyewe, mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wote na angalau idara moja au mbili ilianza Septemba 2016 hadi Februari 2017. Awamu ya pili ilikuwa kati ya Machi 2017 hadi Agosti 2017 ambayo iliwahusisha watendaji wa wizara mbalimbali. Awamu ya tatu ilianza Septemba 2017 hadi Februari 2018 na ya nne Machi 2018 na Agosti 2018.

 

Majaliwa alisema awamu ya tano ambayo ni Septemba 2018 hadi Februari 2020 itakuwa kuhamisha watumishi wa wizara waliobakia jijini Dar es Salaam na ya sita itakuwa ni kati ya Machi 2020 hadi Juni 2020 ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais, Makamu wa Rais watahamia Dodoma.

VIDEO YA MAJALIWA AKIZUNGUMZA KUHAMIA DODOMA

Comments are closed.