The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Agoma Kuingilia Sakata la kina Halima Mdee liko Mahakamani

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) pamoja na Wanachama wa Chama hicho kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Moshi Mkoani Kilimanjaro tarehe 08 Machi, 2023.

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, amekataa kukubali ombi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuingilia kati sakatala la wabunge viti maalum 19, wanaodaiwa kuwepo bungeni kinyume cha sheria, akisema suala hilo liko mahakamani.

Msimamo huo wa Rais Samia ulitolewa Machi 8, 2023, akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mkoani Kilimanjaro, yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).

Ni baada ya baraza hilo na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kumuomba aingilie kati ili wabunge hao waondolewe bungeni kwa madai kuwa hakijawateua.

“La mwisho kwa jina mliloliita (Covid-19), wote wawili wamesema japo kwamba lipo mahakamani lakini mama…, niwaambie tuache mkondo ule uendelee tutazame mbele yanayokuja. Tuachie mkondo ule uendelee, si rahisi mimi hata kama ni Rais kutia mkono huko,” amesema Rais Samia.

Wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee, walifungua kesi Na. 36/2022 katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, kupinga uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama kwa tuhuma za usaliti kufuatia uamuzi wao wa kwenda kuapishwa bungeni jijini Dodoma, kuwa wabunge viti maalum.

Katika kesi hiyo inayosikiliwa mbele ya Jaji Cyprina Mkeha, Mdee na wenzake wanadai hawakujipeleka bungeni, bali waliteuliwa na uongozi wa chama hicho, hivyo wanaiomba mahakama ifanye mapitio dhidi ya mchakato uliotumika kuwavua uanachama wakidai haukuwa halali.

Kwa sasa kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani hapo, ambapo kesho tarehe 9 Machi 2023, mawakili wao wataanza kuwahoji baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Chadema, akiwemo Dk. Azaveli Lwaitama, dhidi ya hati zao za viapo kinzani walizowasilisha mahakamani kujibu malalamiko ya wabunge hao kufukuzwa kinyume cha sheria.

Leave A Reply