The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Aitamani JKT ya Kisasa, Asema Serikali Iko tayari Kusimama nao na Kuwadhamini kwa Kuwapa Mikopo

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hii leo ametinga na mavazi ya kijeshi alipokuwa akiwasili kwenye maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT ) yaliyofanyika mkoani Dodoma.

 

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

 

Rais Samia akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajab Mabele

 

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jacob Mkunda, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Jumaa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk Eliezer Feleshi.

 

Itakumbukwa kwamba JKT ilianzishwa Julai 10, 1963, katika kuelekea siku ya maadhimisho hayo walikuwa na maonyesho mbalimbali Jiji Dodoma, sehemu kubwa wakionyesha bidhaa zinazozalishwa na JKT.

 

Kupitia maadhimisho hayo, Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kwamba anatamani kuona Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linakuwa ni moja kati ya majeshi ya kisasa na  lenye kuwalea vijana wa kitanzania katika misingi ya uzalendo na kuipenda nchi yao.

Rais Samia akikagua Gwaride la Heshima wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 JKT

 

Rais Samia amesema kwamba vijana wanaotoka JKT wanapaswa kuwa wazalendo katika nchi yao na hata wanaobaki katika majeshi na vyombo vya ulinzi wawe watu wenye weledi wa kupigiwa mfano.

 

Aidha, Rais amesema kwamba Serikali ya Jamhuri na Muungano wa Tanzania iko tayari kusimama na JKT na pale itakapowezekana kuwadhamini hata katika mikopo ili waweze kuimarisha vikosi vyao kwenye uzalishaji mali hapa nchini.

 

“Katika miradi mikubwa mmefanya vizuri sana ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, sisi Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na ikibidi mpate mikopo ili kuongeza nguvu ya uzalishaji tuko tayari kuwadhamini,” amesema Rais Samia.

 

 Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 10,2023 wakati akihutubia kilele cha miaka 60 ya JKT katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.

 

Leave A Reply