The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Awataka Wasafirishaji wa Korosho Kwa Malori Kupata Kibali (Picha +Video)

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona tarehe 15 Septemba, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wasafirishaji wa korosho kwa malori mkoani Mtwara kupata kibali maalum kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo.

Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Aidha, Rais Samia amesema lengo la kibali hicho ni kuweza kupata takwimu sahihi za korosho zinazosafirishwa kutoka mkoani humo kwani wapo wafanyabiashara wanaokwepa kusafirisha kwa njia ya bandari.

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Mkoani Mtwara wakiwa katika uwanja wa Nangwanda Sijaona kwa ajili ya kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia tarehe 15 Septemba, 2023.

Rais Samia ameagiza kutumika kwa eneo maalum bandarini lililotengwa kwa ajili ya kupitisha korosho na nafaka nyingine kwa kuwa halitumiki ipasavyo kwa kisingizio cha uchafuzi unaosababishwa na makaa ya mawe.

Rais Samia amemuagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwashughulikia wafanyabiashara wanaochakachua korosho njiani wanaposafirisha kwa malori kwa minajili ya kupata faida kubwa ambapo huathiri ubora wa korosho kwenye soko la dunia.

Wabunge, Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Nangwanda Sijaona tarehe 15 Septemba, 2023.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amezitaka Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa nchini kushughulikia na kuipa kipaumbele migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo yao.

Awali, Rais Samia alikagua miradi ya maendeleo ikiwemo uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, chujio la maji la Mangamba, ukarabati wa kiwanja cha ndege, barabara ya Mtwara-Mnivata (km 50) na kukagua shughuli za uimarishwaji wa bandari.

Leave A Reply