The House of Favourite Newspapers

Rais wa Fifa achukua Ushauri wa Championi, Aahidi Kuufanyia Kazi

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino akiwa na Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally.
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), liliamua kufanya mkutano wake mkuu nchini Tanzania ikiwa ni nchi mbili tu zilizopata nafasi hiyo, barani Afrika.
Nigeria na baadaye Tanzania na hii imekuwa ni mara ya kwanza mkutano huo kufanyika nchini kwa mara ya kwanza huku kukiwa na nchi zaidi ya 48 za Afrika, haujawahi kufanyika.
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino.
Si vibaya kusema lilikuwa ni jambo zuri kwa kuwa wakati wa mkutano huo, pamoja na wajumbe mbalimbali akiwemo Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Caf), Ahmad Ahmad, ambao wote pia wamepata nafasi ya kuitembelea Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano ikiwakilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Hakika ni jambo jema, jambo zuri na linalofungua mwanga mwingine katika mpira wetu wa Tanzania na huenda ni wakati mwingine wa kuanza upya na kufikiria tofauti kwamba tunastahili kupambana kwa nia chanya kuusaidia mpira wetu.
Infantino anajulikana kutokana na msimamo wake alioingia nao katika uongozi, moja ikiwa ni kupambana na rushwa na kuweka uwazi.
Kikao kikiendelea huku mhariri Mtendaji wa Global Publ;ishers, Saleh Ally (aliyevaa shati jeupe kushoto) akiendelea kumsikiliza Rais wa Fifa Infantino.
Akiwa anazungumza na waandishi wachache wa habari waliochaguliwa kufanya naye mahojiano, alisema Fifa sasa imeweka uwazi kwa kuwa kila fedha yake inayoingia inajulikana inatokea wapi na inayotoka inajulikana iendako.
Hii alikuwa akionyesha namna ambavyo wamefanikiwa kuitoa Fifa na kurudi tena kuwa shirikisho la soka badala ya genge la wahuni kama ilivyokuwa hapo awali na hili TFF wanapaswa kulishikilia kwa kuwa bado kuna matatizo mengi ndani ya shirikisho hilo na kabla lilifanywa ni “genge la maswahiba” na watu kufanya wanavyotaka.
Huenda TFF ilikuwa na nafasi ya kufanya madudu kutokana na urafiki wake na Caf yenye wahuni na wababaishaji wengi pia Fifa yenye watu waliokuwa wamejazana kwa ajili ya matumbo yao kwa lengo la kutaka kuonyesha nguvu zao kwa faida zao.
Waziri Mkuu, Majaliwa akipokea Logo ya Fifa kutoka kwa Infantino.
Sasa mambo yamebadilika na bahati nzuri, Infantino ameonyesha namna alivyo na imani kubwa na Rais wa TFF, Wallace Karia na Leodeger Tenga ambaye hakika tunaujua utendaji wake hata kama alikuwa na makosa yake machache kama mwanadamu.
Maneno ya Infantino hakika yanaonyesha mwanga na yanaona mbele naye ameonyesha kuwa na imani kubwa na Afrika kwa kipindi kifupi tena kuliko rais yeyote aliyewahi kuongoza Fifa, ndiyo maana kabla kwa mwaka misaada iliyopelekwa Afrika ilikuwa ni dola milioni 25, lakini sasa imefikia dola milioni 100 na hii inaonyesha kweli sasa Afrika iko katika mpango dhabiti wa maendeleo.
Kumbuka ameiongezea Afrika kutoka timu tano hadi tisa zinazoshiriki Kombe la Dunia na yeye amesema uongozi wa awali, ulikuwa ukisema tu na yeye amepitisha uamuzi.
Infantino ameonyesha ni mtu anayekubali ushauri, kwani Gazeti la Championi lilikuwa ni chombo pekee cha habari kilichoomba kutoa ushauri kwake katika masuala mawili, moja likiwa ni kuishawishi Serikali ya Tanzania nayo kusaidia kwa kuingiza fedha katika soka pia.
Pili suala la kuwasaidia waandishi kujifunza zaidi kuhusiana na masuala ya soka na rushwa, hasara na faida na mengine mengi kama biashara na kadhalika kwa kuwa ndiyo wamekuwa wale “wanaofukua” makaburi na kusababisha mabadiliko.
Infantino mbele ya Karia, Tenga na wanahabari wengine, alionekana kufurahia akisisitiza kwamba ni wazo zuri na atalifanyia kazi.
Infantino akimkabidhi zawadi ya jezi Waziri Mkuu, Majaliwa baada ya kikao chao na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar.
TFF imeaminika na Karia na Tenga wanapaswa kupongezwa lakini kikubwa wanachotakiwa kufanya ni kubadilika kwa vitendo kama ambavyo ameanza kuonyesha Infantino.
Ili aiamini zaidi Tanzania, lazima kuwe na utekelezaji na tunapaswa kuwaunga mkono hasa sehemu yenye maumivu kwa nia ya kusaidia mpira wa Tanzania ambao ulikuwa jalalani miaka nenda rudi.
Fifa kupitia Infantino na Caf kupitia Ahmad, wameonyesha kuvutiwa na serikali ya awamu ya tano inavyotekeleza mambo. Yaani ni utendaji na si maneno tu na wamesisitiza ni moja ya sehemu ya wao kuja nchini kufanya mkutano wao.
Maana yake, kama Fifa na Caf zinaonyesha imani kwa serikali yetu ni jambo la kujivunia kwetu lakini serikali nayo huu ni wakati mwafaka wa kuingiza fedha zake katika soka.
Mfano Yanga na Simba ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa kama wawakilishi wa taifa letu, wanapaswa kusaidiwa kwa kiasi cha fedha na hili itaonyesha namna ambavyo wawakilishi wanaweza kupewa nguvu.
Rais wa FIFA,Gianni Infantino (wa kwanza kushoto), akiwa kwenye pozi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chake na waandishi wa habari, jana ofisini kwake Ikulu jijini Dar. Kulia ni Rais wa Caf, Ahmad Ahmad.

 

Lakini serikali bado ina nafasi ya kuingia na kusaidia soka ya vijana na wanawake kwa kuzishawishi kampuni kadhaa kudhamini lakini kuonyesha inataka usimamizi wa karibu wa matumizi ya fedha ili ziwe na faida katika kile kilicholengwa. Hakika hakuna kinachoshindikana, kumbukeni Tanzania ni yetu sisi.
Makala na Na Saleh Ally, Championi

Comments are closed.