The House of Favourite Newspapers

Rais Zelensky Alihutubia Bunge La Uingereza

0

RAIS Volodomyr Zelensky, amelihutubia Bunge la Uingereza (House of Commons) kwa njia ya mtandao na kuahidi kwamba watapambana mpaka kumshinda Rais Vladimir Putin ambaye majeshi yake yameivamia Ukraine yakiendelea kusababisha uharibifu mkubwa nchini humo.

“Tutapigana naye baharini, tutapigana naye angani, misituni na mitaani, kamwe hatutakubali kushindwa,” alisema Zelensky katika hotuba hiyo ya kihistoria, akinukuu maneno ya Sir Winston Churchill aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyoyatoa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

 

Wabunge wa Uingereza, wameonesha kuguswa sana na hotuba hiyo ambapo mara kadhaa walikuwa wakimpigia makofi kwa nguvu na kusimama kama ishara ya kumuunga mkono rais huyo wa Ukraine.

 

Zelensky ameufananisha uvamizi uliofanywa na Urusi nchini Ukraine sawa na uvamizi uliofanywa na Ujerumani iliyokuwa chini ya sera za kinazi za Adolf Hitler katika ardhi ya Uingereza wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

 

Ameongeza kwa kusema: “Hatutasalimu amri na hatutapoteza vita hii. Tutapigana mpaka mwisho, baharini, angani, tutaendelea kuipigania nchi yetu kwa gharama zozote na kueleza kuwa Ukraine inapigana vita ambayo haijaianzisha na haiitaki lakini hawapo tayari kupoteza kile ambacho tayari wanacho.

 

Amewaambia wabunge wa Uingereza kwamba kama ambavyo Waingereza walipambana na uvamizi wa Ujerumani, ndivyo wananchi wa Ukraine wanavyopambana na uvamizi wa Urusi katika ardhi yao na kusema mpaka sasa watoto zaidi ya 50 wameshapoteza maisha yao kutokana na uvamizi wa Urusi.

 

Baada ya Zelensky kumaliza kulihutubia bunge hilo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson amewaambia wabunge hao kuwa Uingereza na washirika wake wataendelea kutoa misaada ya hali na mali kwa rafiki zao wa Ukraine ikiwemo silaha ili waendelee kuilinda nchi yao.

 

Ameongeza kwamba Uingereza itaendelea kuiwekea vikwazo Urusi kwa kuacha mara moja kununua mafuta kutoka nchini humo na wataendelea kuisaidia Ukraine kuhakikisha Urusi inafeli katika uvamizi huo.
Pia Poland imesema ipo tayari kutoa ndege 28 za kivita kuisaidia Ukraine kupambana na mashambulio ya anga ya majeshi ya Urusi.

 

Marekani nayo imesema inakusudia kupiga marufuku kuingizwa mafuta yanayotoka Urusi nchini humo katika hatua ya mwendelezo wa kuiwekea Urusi vikwazo kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

 

Uingereza na Ujerumani pia zipo kwenye mkakati wa kuiwekea vikwazo sekta ya nishati kutoka Urusi ikiwa ndiyo sekta pekee ambayo mpaka sasa imebaki kuwa mhimili wa kiuchumi unaotegemewa na Urusi.

 

Boris amesema mataifa hayo mawili yamekubaliana kutafuta mbadala wa gesi ya Urusi kabla hawajapitisha uamuzi wa kuzuia mafuta na gesi kutoka katika taifa hilo kubwa lililopo Ulaya Mashariki.

 

Wakati hayo yakiendelea, Serikali ya Ukraine imesema mpaka sasa imefanikiwa kuwaua wanajeshi 12,000 wa Urusi na kuharibu zaidi ya vifaru 300 vya kijeshi.

 

Kwa upande wa Urusi, imeendelea na mashambulizi katika miji mbalimbali mikubwa nchini humo na hapo jana, jumla ya watu 21 wakiwemo watoto wawili, walipoteza maisha nchini Ukraine kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Urusi.

Leave A Reply