The House of Favourite Newspapers

Rasmi Mfaransa Out Simba Sc … Sh Milioni 90 Zatajwa

Kocha wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre akiongea na kocha wake wa viungo enzi wakiwa Simba.

 

RASMI sasa Kocha wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre, ametimuliwa Msimbazi. Hii ni baada ya Championi kunasa taarifa hizo takriban wiki mbili kabla.

 

Lechantre, ambaye alitua Simba Januari, mwaka huu na kuanza mechi yake ya kwanza Januari 28, ametimuliwa baada ya kuiongoza Simba kwa mechi 15 tu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi cha timu ya Simba.

 

Kisa kikubwa cha kutimuliwa kama ilivyoandikwa katika gazeti bora la michezo Tanzania, Championi, ni madai yake ya mshahara wa Sh milioni 90 kila mwezi ili asaini mkataba mpya.

 

Pamoja na sababu hiyo, Lechantre ambaye alikwenda Kenya kuiongoza Simba katika michuano ya SportPesa Super Cup, jana kabla ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya Kakamega Home Boys, kocha huyo aligoma kuiongoza timu akidai mkataba mpya.

 

Taarifa ambazo Championi lilikuwa nazo ni kwamba, Lechantre aliondoka Bongo akiwa amekubaliana na mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwa atapewa mkataba baada ya kumalizika kwa michuano ya SportPesa Super Cup.

 

Lakini jana, alipomuona Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alimlalamikia kuwa hana mkataba na akadai hawezi kuendelea kuiongoza timu hiyo akiwa hana mkataba.

 

Baada ya mabishano ya muda mrefu, Try Again alikubali kwamba asiiongoze Simba jana dhidi ya Kakamega, na badala yake Mfaransa huyo akaenda kukaa jukwaani na mashabiki akiwa amenuna, huku msaidizi wake Masoud Djuma akiiongoza Simba kutinga fainali kwa mikwaju ya penalty 5-4.

 

Baada ya kugoma kuiongoza timu hiyo jana, ndipo ikaelezwa kuwa Try Again akachukua uamuzi wa kumng’oa rasmi Mfaransa huyo ambaye ameiongoza Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, akichukua mikoba ya Mcameroon, Joseph Omog ambaye alimaliza mzunguko wa kwanza akiwa hajapoteza mechi yoyote.

 

Championi linafahamu kuwa Mfaransa huyo asingeweza kuendelea kuwa kocha wa Simba kutokana na Wekundu hao kukerwa na tabia yake ya kupenda fedha kupita kiasi, huku pia wakiwa hawafurahishwi na aina ya soka lake.

 

Simba pia ilikerwa na namna kocha huyo alivyowatumia wachezaji wake, wengine akiwachezesha katika nafasi zisizo zao, mfano straika Nicholaus Gyan ambaye alikuwa anachezeshwa kama beki wa pembeni chini ya Lechantre.

 

Hata hivyo, Championi linafahamu kuwa Simba pia haikuwa ikipendezwa na misimamo ya kocha huyo ambaye alikuwa hataki kuingiliwa katika mipango yake ya kikosi.

 

Championi lilimpata Kaimu Rais wa Simba, Try Again, jana mchana akathibitisha kuwa kocha huyo anaondoka lakini akakataa kufafanua zaidi akidai atazungumza mengi kuhusu ufafanuzi huo baadaye.

 

“Akitoka hapa, kocha atakwenda kwao, kuna matatizo yametokea. Kwa sasa siwezi kuyaeleza kwa kirefu, nitayatolea ufafanuzi baada ya harakati hizi,” alisema Try Again.

 

Wachezaji wa Simba, jana walishtushwa kutokana na kutokumuona kocha wao katika benchi la ufundi muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya Kakamega Home Boys.

 

Kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima, alisema baada ya kushinda mechi ya jana na kutinga fainali, wachezaji wa timu hiyo walikwenda jukwaani kushangilia na Lechantre ili kumpa heshima yake kutokana na mchango wake katika Klabu ya Simba.

 

“Tulikwenda kushangilia kwa kocha kama kumuonyesha heshima, matatizo yao na uongozi hayatuhusu, maana tuliuliza kwa nini hayupo, tukaambiwa mwenye macho haambiwi tazama,” alisema Niyonzima.

 

Lechantre anaondoka Simba akiwa ameshinda mechi 10, ikiwemo dhidi ya mahasimu wao, Yanga huku akiwa ametoa sare nne na kufungwa mechi moja katika Ligi Kuu Bara.

 

Msaidizi wake, Mtunisia, Aimen Mohammed Habib, atafuatana naye kuondoka Simba, kwani naye jana aligoma kuiongoza Simba dhidi ya Kakamega.

Simba itaendelea kuwa na Djuma kama kocha mkuu huku ikiendelea kusaka kocha wa kuvaa viatu vya Lechantre.

STORI NA MUSA MATEJA | GPL – KENYA

Comments are closed.