The House of Favourite Newspapers

Rekodi ya Mbelgiji Simba ni noma

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, Jumatano iliyopita, alitimiza siku 19 ndani ya kikosi hicho akifanya kazi bila kuwa na kocha msaidizi, lakini amefanikiwa kufanya makubwa.

 

Simba Oktoba 5, mwaka huu ilimuondoa kikosini mwake Kocha Msaidizi Mrundi, Masoud ambaye zilikuwa haziivi na Mbelgiji huyo huku akiwa na shutuma kuwa alikuwa akiwatumia wachezaji kupanga matokeo.

 

Hata hivyo, tangu siku hiyo ambayo Djuma alipofungashiwa virago vyake klabuni hapo, Aussems amefanikiwa kuiongoza Simba katika mechi tatu za ligi kuu na kupata ushindi mnono ukilinganisha na ule ambao timu hiyo ilikuwa ikiupata wakati Djuma akiwa bado ndani ya timu hiyo.

 

Mechi hizo tatu ambao Aussems ameiongoza Simba bila ya kuwa na kocha msaidizi ni dhidi ya African Lyon ambapo ilishinda mabao 2-1, Stand United (3-0) pamoja na Alliance FC (5-1). Katika mechi hizo tatu, Simba imefanikiwa kujikusanyia jumla ya mabao 10 na kufungwa mawili.

 

Matokeo hayo yanatofautiana na yale ambayo iliyapata katika mechi sita ilizocheza wakati Djuma akiwa bado ndani ya Simba. Katika mechi hizo Simba ilifanikiwa kushinda tatu, ikatoka sare mbili lakini pia ikafungwa mchezo mmoja huku ikifanikiwa kufunga mabao sita tu katika mechi hizo na kufungwa mawili.

 

Akizungumza hilo, Aussems alisema: “Mwanzo tulikuwa tukipata ushindi wa mabao kidogo kwa sababu wachezaji walikuwa bado hawajazoeana vizuri lakini kwa sasa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo wanazidi kuzoeana, kwa hiyo hakuna kitu kingine zaidi ya hilo.

 

“Niwapongeze tu wachezaji wangu kwa kazi kubwa wanayoifanya sasa na niwaombe waendelee kujituma zaidi mazoezini ili waweze kuwa fiti muda wote,” alisema Aussems.

 

Naye kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude amezungumzia ishu hiyo na kusema: “Kuhusiana na rekodi ya kushinda mabao 10 ambayo tumeiweka hivi karibuni katika mechi tatu tulizocheza dhidi ya African Lyon, Stand United pamoja na Alliance FC hakika ni ya kipekee.

 

“Nimpongeze pia kocha wetu, Aussems kwa jitihada zake ambazo amekuwa akizifanya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote, ukilinganisha hapo awali ambapo tulikuwa tunashinda kwa idadi ndogo ya mabao.”

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

Comments are closed.