The House of Favourite Newspapers

Ripoti Kamili Ya Mchungaji Aliyeoa Mke wa Muumini, Aongea na Risasi

0
 Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo, Japhes Josephat (kulia) akiwa na mke aliyemuoa.

STORI: Gabriel Ng’osha | Risasi Jumamosi | Habari

KAGERA: Tukio la Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo, Japhes Josephat kudaiwa kumuoa mke wa muumini wake kwa madai ya kuoteshwa na Mungu wake, ndiyo habari ya mjini ya kushangaza na Risasi linakupa ripoti kamili. Mtumishi huyo wa Mungu alifanya jambo hilo hivi karibuni kwenye Kijiji cha Ndama, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera na kuushangaza umma kwani mwanamke aliyemuoa, Domina Damian ni mke halali wa muumini wa mchungaji huyo aliyefahamika kwa jina la Donath Appolo.

RISASI LACHIMBA

Kutokana na habari hiyo kuonesha kuvuta hisia za watu wengi, gazeti hili lilifika Kijiji cha Ndama kwa njia ya mtandao na kuzungumza na mchungaji mwenyewe pamoja na watu mbalimbali ambao walionesha kushangazwa na uamuzi wa ‘mchunga kondoo’ huyo huku mwenye mke akionesha kukubaliana na maono yake.

Mke aliyeolewa na mchungaji.

WADAKWA NA POLISI, WAACHIWA

Ilielezwa kuwa, Jeshi la Polisi wilayani Karagwe lilimkamata mchungaji huyo pamoja na wenzake wawili lakini baada ya kohojiwa waliachiwa kwani hakukuwa na mlalamikaji kufuatia mume wa Domina kubariki mtumishi huyo amchukue mkewe na yeye Mungu atamjaalia atapata mwingine.

WANANCHI WACHARUKA

Baada ya kubainika kuwa mtuhumiwa ameachiwa huru, wanakijiji wa Ndama waliweka kikao na kuazimia kuwa mchungaji huyo ahame kijiji chao kwani kawaaibisha. “Tuliiomba serikali kupitia mkuu wa wilaya kumhamisha mchungaji pale kijijini kwa sababu wananchi walikuwa wana hasira sana, waliona ni jambo la aibu ambalo haliwezi kuvumiliwa,” alisema mmoja wa wanakijiji aliyefahamika kwa jina la Johnson.

Mchungaji na mke wa muumini wakiwa chini ya ulinzi.

MWANAKIJIJI MWINGINE

“Tulipokea kwa mshangao sana tukio zima la mchungaji huyo pamoja na waumini wake, kwani tuliamini makanisa ya kilokole yanakataza maovu mbalimbali sasa inakuwaje mchungaji anamuoa mke wa muumini wake tena akiwa hai? “Watu wamehamaki sana, kama mkuu wa wilaya asingekuja naamini kungeweza kutokea jambo baya zaidi, watu walikuwa wana hasira sana kwa yale yaliyofanywa na mchungaji,” alisema Peter.

Mchungaji huyo akiongea jambo.

MCHUNGAJI AFUNGASHA VIRAGO

Kutokana na wanakijiji kuja juu, imeelezwa kuwa juzikati mchungaji huyo aliamua kufungasha virago vyake na kuhamia kijiji kingine ambacho hakiko mbali sana na sehemu aliyokuwa akitolea huduma.

ATEMWA UCHUNGAJI

Kwa mujibu wa mchungaji kiongozi wa   kanisa hilo, ngazi ya wilaya, Denis Bilalo mchungaji huyo licha ya kuhama eneo hilo pia wamemsimamisha kutoa huduma ya kiroho. “Sisi kama uongozi wa kanisa ngazi ya wilaya tumetengua uchungaji wake, kwa hiyo Japhes siyo mchungaji tena wa kanisa letu na hatakiwi kutoa tena huduma. “Kitendo alichokifanya ni kinyume na maandiko matakatifu, ni kinyume kabisa na mipango ya Mungu,” alisema kiongozi huyo.

DIWANI ATIA NENO

Diwani wa Kata ya Ndama, Edward Mpaka alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai ni jambo la kushangaza sana kwa kiongozi wa dini kufanya kitu kama hicho. “Ninachokiona mimi labda ni kupitiliza kwa imani lakini pia kuwepo kwa tatizo la kisaikolojia kwa wahusika kwa sababu haiwezekani mwenye mke akaunga mkono mkewe kuolewa. “Ushauri wangu kwa jamii ni kuwa makini na baadhi ya viongozi wa dini kwani hata
Biblia inatuambia kuwa manabii wa uongo watakuja,” alisema.

MSIKIE MCHUNGAJI Gazeti la Risasi Jumamosi lilifanya jitihada za kuwasiliana na mchungaji ‘aliyechafua hali ya hewa’, Japhes ambapo hakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema kwamba kwake yameisha na anachofanya ni kusikiliza alichoambiwa na Mungu wake. “Sina wakati wa kuyazungumzia hayo sasa kwa sababu yameisha, kama hukupata nafasi ya kuwasikia wenzako basi, namsikiliza Mungu wangu,” alisema mchungaji huyo.

MCHUNGAJI ANA MKE NA WATOTO WATANO

Risasi limetonywa kuwa, mchungaji huyo aliwahi kuwa na mke ambaye alizaa naye watoto watano.

NDOA YA MUUMINI INA WANNE

Aidha, mke ambaye amemuoa kwa madai ya kuoteshwa ana watoto wanne kwa mumewe ambaye anaunga mkono maono ya mchungaji wake.

Leave A Reply