The House of Favourite Newspapers

RIPOTI YA CAG KUWASILISHWA BUNGENI LEO

Leo Jumatano Aprili 10, 2019 Bunge la Tanzania litawasilishiwa hati ya Ripoti  ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

 

Orodha ya shughuli za Bunge leo Jumatano, Aprili 10 inaonyesha taarifa hiyo ya fedha ya mwaka wa fedha 2017/18 itawasilisha bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisa ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiwa ni siku ya saba tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti Aprili 2, 2019.

 

Hata hivyo orodha hiyo inaweza kubadilika.

 

Wakati taarifa hiyo ikiwasilishwa, jana Jumanne, Aprili 9 jioni ofisi ya CAG ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa leo Profesa Assad atakuwa na mkutano na waandishi kueleza yaliyomo katika taarifa yake ya ukaguzi.“Nawakaribisha katika ukumbi wa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (Naot) ghorofa ya pili. Jengo lipo nyuma ya jengo la hazina (Dodoma). Karibuni nyote msihofu,” Inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya mwaliko.

 

Hata hivyo, siku zote taarifa hiyo baada ya kuwasilishwa bungeni, CAG hukutana na wanahabari katika ukumbi wa Bunge kueleza yaliyomo katika ripoti yake ya ukaguzi, huenda safari hii ameamua kufanyia ofisini kwake kutokana na azimio la Bunge la kutofanya naye kazi.

 

Jana Mwananchi lilizungumza na wabunge na kueleza kuwa wataijadili ripoti yake ya ukaguzi lakini si kumuona msomi huyo bungeni.Wamesema kutokana na ofisi ya CAG kuwa na watendaji wengi, anaweza kutuma wasaidizi wake kuja bungeni kwa ajili ya kuiwasilisha taarifa hiyo.

 

Wakati wabunge hao wakitoa kauli hiyo kumekuwa na hali ya sintofahamu kuhusu sakata hilo ambako juzi kwa nyakati tofauti Mwananchi lilizungumza na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kama Bunge limepata ripoti hiyo na kujibiwa kuna hana taarifa huku Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai akitaka atafutwe Spika Job Ndugai ambaye yupo nje ya nchi na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.

 

Wakizungumzia ripoti hiyo mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto amesema hana shida na ripoti hiyo kwa sababu taarifa nzima ni mali ya Serikali si mtu binafsi.Amebainisha kuwa uwepo na saini ya Profesa Assad katika taarifa hizo za ukaguzi haina maana  kuwa ndiyo haifai badala yake wataijadili na kuitendea haki.”

 

Hapa tukubaliane kuwa yeye ndiyo hatakiwi kuja mbele ya kamati au Bunge, akae huko na amtume msaidizi wake au mtu mwingine ambaye atajibu maswali,” amesema Mwamoto.Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka amesema shida yao ni Profesa Assad na si taarifa yake.

 

Amebainisha kuwa CAG hatakiwi kuitwa hata kwenye kamati kwa ajili ya kutoa ufafanuzi ila anaweza kumtuma mtu mwingine.Mbunge huyo ambaye amejiunga na CCM akitokea CUF, amesema anashangazwa na mtu msomi kama Assad kukituhumu chombo muhimu kama Bunge huku akitarajia kupata ushirikiano.

 

Naye mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde amesema taarifa hiyo wanaisubiri kwa hamu kubwa na wataijadili bila kinyongo.”Watu watambue kuwa hatukatai taarifa ya CAG, kikubwa hapa ni kuwa hatumtaki Profesa kwa hiyo ile ni taasisi anaweza kumleta mtu yeyote kwa niaba yake,” amesema Lusinde.

 

Hata hivyo, amesema wakati msomi huyo analituhumu Bunge kuwa ni dhaifu, tayari alishamaliza kazi ya ukaguzi hivyo haitakuwa sahihi ripoti yake kukataliwa.Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi amesema wanaisubiri ripoti hiyo kwa kuwa walishapata taarifa imeibua madudu ya kutisha katika halmashauri.

 

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliliambia Mwananchi kuwa azimio la Bunge ilikuwa kutofanya kazi na CAG linatakiwa kuangaliwa kwa umakini.

 

“CAG ni ofisi sio mtu, unaona tunavyojichanganya. Nadhani viongozi wameona kuna kosa limetokea mahali fulani ndio maana Spika kasema kilichoazimiwa ni kutofanya kazi na Profesa Assad, azimio halikumtaja Assad lilimtaja CAG,” amesema Selasini.

Comments are closed.