The House of Favourite Newspapers

Saa 2 za Kessy mazoezini Yanga

0

KESSY (2)    Beki wa kulia mpya wa timu ya Yanga, Hassan Kessy.

Wilbert Molandi na Mohammed Mdose

AKIRIPOTI kwa mara ya kwanza kwenye mazoezi ya Yanga, beki wa kulia mpya wa timu hiyo, Hassan Kessy na kiungo mshambuliaji, Juma Mahadhi jana Jumanne walitumia dakika 120 (sawa na saa 2) kujifua na kikosi hicho.

Kessy ametua kuichezea Yanga hivi karibuni akisaini mkataba wa miaka miwili akitokea Simba pamoja na Mahadhi aliyetokea Coastal Union ya Tanga kila mmoja akisaini kwa dau la Sh milioni 40.

KESSY (1)

Kessy akiweka sawa viatu vyake kabla ya mazoezi.

Kabla ya mazoezi hayo kuanza, beki huyo pamoja na Mahadhi walifika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam wanapofanyia mazoezi hayo saa 2:30 asubuhi wakiwa na basi la timu hiyo wakiongozana na Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh.

Mara baada ya kufika hapo, wachezaji hao wapya walisalimiana na wenzao, kisha kuvaa vifaa vyao vya mazoezi na kwenda kutambulishwa kwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi aliyesimamia mazoezi hayo pamoja na kocha wa makipa, Juma Pondamali.

KESSY (5)

…Akiwa na wachezaji wenzake mazoezini.

Baada ya kutambulishwa beki huyo, alizungumza na kocha huyo kwa dakika tano pamoja na Mahadhi baada ya hapo akaanza mazoezi pamoja na wenzao saa 3:00.

Zoezi la kwanza kuanza nalo Kessy na Mahadhi lilikuwa ni kuzunguka uwanja mzima kwa taratibu na baadaye kukimbia mbio fupi na kisha ndefu  kwa dakika 45 huku beki huyo akionekana kufanya kwa ufasaha na mara nyingi alikuwa mbele.

Baada ya hapo, walianza kufanya mazoezi ya kupigiana pasi ‘open space’ wachezaji wote kwa kucheza nusu uwanja huku Kessy akionekana kupiga pasi nyingi kwa umakini mkubwa sawa na ilivyokuwa kwa Mahadhi.

KESSY (3)

Akifunga kamba za viatu.

Kessy, licha ya kukaa nje ya uwanja muda mrefu kwa kusimamishwa na uongozi wa Simba wakati Ligi Kuu Bara ikiendelea kwa kosa la kumchezea rafu ya makusudi mshambuliaji wa Toto Africans, Christopher Edward, alionekana kuonyesha umakini wa upigaji wa pasi, kumiliki mpira na kukaba pale alipotakiwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, kuna wakati wachezaji wenzake ambao wengi walikuwa wa timu ya vijana walionekana kufarahishwa na jinsi Mahadhi naye alivyokuwa akitoa pasi safi ambazo zinafika kwa walengwa.

Baada ya hapo, Mwambusi aliwataka wachezaji hao kufanya mazoezi ya viungo kwa ajili ya kunyoosha miili yao wakitumia dakika 30, kisha kumaliza mazoezi hayo na kuondoka uwanjani hapo.

KESSY (4)

Mara baada ya kuondoka uwanjani hapo, Kessy alitua makao makuu ya klabu na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa timu hiyo.

Alipoulizwa Kessy kuhusiana na mazoezi hayo akifanya kwa siku ya kwanza alisema: “Kwanza kabisa nashukuru kwa mapokezi makubwa niliyoyapata Yanga, najiona kama mwenyeji kutokana na baadhi ya wachezaji kujuana nao wakiwa wanaichezea timu ya taifa, Taifa Stars.

“Nimeanza mazoezi leo (jana), lakini sijawaona baadhi ya wachezaji niliozoeana nao sana kama vile Abdul (Juma) na Msuva (Simon), hata hivyo ninajisikia furaha sana kuwepo kwenye timu yenye amani,” alisema Kessy.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mholanzi Hans van Der Pluijm alitarajiwa kutua nchini jana saa 4:00 usiku kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda akitokea nyumbani kwake Ghana.

 

Leave A Reply