The House of Favourite Newspapers

SABABU 10 ZA MAUMIVU KWA MJAMZITO.

LEO nitakufahamisha sababu kumi (10) za maumivu ya tumbo wakati wa miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito. Maumivu ya tumbo ni mojawapo ya matatizo mengi yanayolalamikiwa na wajawazito walio wengi.

Kuna matatizo mengi yanayosababisha maumivu kwa wanawake wenye ujauzito. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba hali yoyote ambayo husababisha maumivu kwa mgonjwa asiyekuwa na ujauzito inaweza pia kutokea kwa mjamzito, ingawaje historia na uchunguzi vinaweza kuwa tofauti.

Kwa asili kutathmini maumivu ya tumbo kwa mama mjamzito, kuna changamoto nyingi kwa sababu kichefuchefu, kutapika na maumivu ya tumbo hujitokeza mara nyingi kwa wengi wao.

MIMBA NJE YA MFUKO

Mgonjwa ambaye mimba imetunga nje ya mfuko wa kizazi kipimo cha Ultra-Sound ni lazima kitumike na kitaonesha mambo mengi, ikiwa ni pamoja na majimaji na uchafu ndani ya mfuko huo.

Mimba iliyotunga nje ya mfuko wa uzazi ni tatizo linaloongoza kusababisha maumivu kwa akina mama wengi. Tatizo hilo linaweza kubainika kwa kutumia Ultra-Sound na kipimo cha homoni kiitwacho HCG.

Hata hivyo, tatizo hili linatibika kama dharura kwa mama kufanyiwa upasuaji.

KIINITETE KUJIPANDIKIZA

Kiinitete kinapojipandikiza kwenye kuta za ndani za mfuko wa uzazi kinaweza kusababisha maumivu makali ya tumbo kwa mjamzito. Maumivu haya huchukua siku moja hadi mbili. Lakini pia pamoja na tatizo hilo, kiasi kidogo cha damu kinakuwa kinatoka ukeni.

Mara nyingi damu hiyo hutokea kati ya siku sita hadi 12 baada ya tarehe inayohisiwa mimba kutungwa. Mara nyingi kipindi hiki hukaribiana na siku ambayo mwanamke anatarajiwa kuingia katika siku zake.

Hivyo, wagonjwa mara nyingi hufanya makosa kwa kufikiri kuwa wameingia katika siku zao kama kawaida.

MFUKO WA UZAZI KUTANUKA

Mfuko wa uzazi unapotanuka wakati mtoto anakua tumboni, unaweza kusukuma viungo vingine kando ndani ya tumbo na kusababisha maumivu. Hapo pia kunaweza kujitokeza upungufu wa damu na kitu kinachoitwa kitaalam Leukocytosis, mambo ambayo ni kawaida kwa mjamzito na vikawa siyo viashiria vya upungufu wa damu au maradhi.

KINACHOSHIKILIA MFUKO WA UZAZI

Sababu nyingine ya maumivu husababishwa na kitu kinachoitwa kitaalam Round Ligament.

Ligament ndiyo inayoshikilia mfuko wa uzazi. Mfuko wa uzazi unavyozidi kukua, ligament huvutika na kusababisha maumivu makali kwa mama mjamzito. Mara nyingi daktari hutoa dawa za maumivu kwa mama mjamzito kumpunguzia maumivu.

KUTOKA KWA MIMBA

Sababu nyingine ni kutoka kwa mimba. Mimba inaweza kutoka yenyewe au kutolewa kwa makusudi. Tatizo hili huambatana na maumivu na kuvuja damu. Hata hivyo, utoaji mimba usiokuwa salama unaongoza kusababisha vifo vya akina mama katika nchi zinazoendelea.

UVIMBE KWENYE MIRIJA YA MAYAI

Wakati mwingine uvimbe huu wa kwenye mirija ya mayai hupasuka au kujizungusha. Hata hivyo, unaweza kupungua na usipopungua unaweza kuondolewa kwa njia ya upasuaji hasa wakati wa muhula wa pili wa ujauzito.

KUJIZUNGUSHA KWA MIRIJA YA MAYAI

Sababu nyingine ya maumivu ya tumbo kwa mjamzito ni kujizungusha kwa mirija ya mayai kitaalam Ovarian Torsion. Hii hujitokeza mara chache.

Uvimbe kwenye mfuko wa uzazi pia husababisha maumivu hasa unapokuwa mkubwa. Tatizo hili linaweza kusababisha ujauzito kutoka hasa katika miezi ya awali.

KIDOLE TUMBO

Kidole tumbo (Appendicitis) kinaweza kusababisha maumivu ya tumbo kwa mjamzito na hujitokeza kwa uwiano sawa kama wanawake ambao hawana ujauzito. Matibabu ya ugonjwa huu ni upasuaji. Mara nyingi wanawake wengi hupata uchungu baada ya upasuaji.

Kutokana na mabadiliko ya homoni, wanawake wengi hupata tatizo la mawe kwenye mfuko wa nyongo. Tatizo hili huweza kugunduliwa kwa njia ya kipimo cha Ultra-Sound. Matibabu hutegemea na dalili na uchunguzi wa kidaktari.

UVIMBE MFUKO WA NYONGO

Uvimbe unaoitwa kitaalam Inflammation kwenye mfuko wa nyongo ni tatizo la ghafla linalosababisha maumivu makali ambalo pia hujitokeza wakati wa mimba.

Tatizo hili mara nyingi husababishwa na mawe kwenye mfuko wa nyongo. Dawa za kuua bakteria (Anti-biotics) hutumika katika matibabu ya ugonjwa huu.

MAAMBUKIZI NJIA YA MKOJO

Wanawake wengi wakati wa ujauzito hupata maambukizi kwenye njia ya mkonjo mara kwa mara. Hii ni kutokana na mabadiliko yanayojitokeza wakati huu wa ukuaji wa mimba.

UCHUNGUZI, TIBA NA USHAURI

Ultra-Sound hutumika katika uchunguzi wa maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito. Kongosho, mfuko wa nyongo na kidole tumbo vyote huonekana kwa mama mjamzito. Vipimo vinavyotumia mionzi vitumike tu pale inapohitajika kwa mama mjamzito.

Matibabu ya ugonjwa wa tumbo yatatolewa kulingana na matokeo ya uchunguzi. Kwamba mgonjwa atatibiwa kulingana na tatizo lililogundulika na daktari, hivyo uonapo dalili za kuumwa tumbo, wahi hospitali ukafanyiwe uchunguzi.

Comments are closed.