The House of Favourite Newspapers

SABABU, DALILI ZA UGONJWA WA DEGEDEGE KWA WATOTO

UGONJWA wa Degedege (Seizures) ni mojawapo ya maradhi hatari sana kwa watoto na huogopesha sana wazazi na walezi wengi.  

 

Katika hili kuna dhana tofautitofauti zilizojengeka miongoni mwa wanajamii, ambapo baadhi huamini degedege ina uhusiano na mambo ya ushirikina na kwamba huweza kutibiwa kwa njia za namna hiyo, jambo ambalo siyo kweli.

 

Wazazi na walezi wenye imani za namna hii hukataa kuwapeleka watoto wao hospitali wakiamini kuwa watakufa iwapo wataachwa wapate matibabu ya hospitali. Dhana nyingine iliyojengeka ni ile ya kuwa degedege ni tatizo linalotokea mara moja tu maishani mwa mtoto kitu ambacho pia si kweli.

 

Aidha wapo pia baadhi ya wanajamii wanaohusisha degedege na ugonjwa wa malaria pekee. Ukweli ni kwamba karibu asilimia 3 ya watoto chini ya miaka 15 hupata degedege, nusu ya hawa hupata degedege linalosababishwa na homa kali. Kwa maana hiyo basi, degedege pia linaweza kumpata mtoto asiye na homa kama kifafa. Inakadiriwa kuwa mtoto mmoja kati ya 100 hupata degedege ya kifafa.

 

DEGEDEGE HUTOKEAJE?

Degedege ni dalili inayoonesha mvurugano katika ufanyaji kazi wa seli za ubongo. Kwa kawaida, seli za ubongo ambazo kwa kitaalamu huitwa neurons huwasiliana kwa njia ya mtiririko wa umeme (electrical impulses).

 

Huu ni mtiririko wa mawasiliano ya umeme wa mwili kati ya seli za ubongo ndiyo unaofanya mwili uweze kufanya kazi ipasavyo. Iwapo basi itatokea kuwepo sababu yoyote ile itakayosababisha mawasiliano kati ya seli za ubongo kutokuwa katika mtiririko sahihi mfano kuwepo msisimko wa mawasiliano, hali hiyo husababisha degedege.

 

Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha mtoto kukumbwa na degedege. Moja ya mambo yanayoweza kusababisha mtoto kupata ugonjwa wa degedege ni kuwepo kwa jeraha katika ubongo, kitaalamu huitwa brain injury, ambalo linaweza kuwa kwa sababu yoyote ile ikiwemo jeraha analopata mtoto wakati wa kuzaliwa, kitaalamu huitwa brain ischemia.

Lakini pia kuna baadhi ya familia ambazo zinakuwa na matatizo ya kimaumbile katika ubongo zinazorithiwa toka kizazi hadi kizazi hasa ugonjwa wa kifafa. Familia za namna hii huwa na watoto ambao hupatwa na ugonjwa wa degedege kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko familia ambazo hazina matatizo haya.

 

Vilevile degedege inaweza kuhusishwa na hali ya mabadiliko ya muda mfupi katika ubongo kama vile joto kali, matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine, amphetamine, viwango visivyo vya kawaida vya sukari na sodium katika damu (electrolytes imbalance) na uwepo wa uvimbe katika ubongo, yaani brain tumor.

 

Sababu nyingine zinazoweza kusababisha degedege ni ugonjwa wa saratani ya ubongo, matatizo ya kimaumbile katika ubongo ya kuzaliwa nayo (congenital brain defects), mashambulizi ya vimelea vya bakteria, virusi, fangasi katika ubongo kama vile ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis).

 

Degedege lisilo na homa (Unprovoked Seizures)

Ni aina ya degedege ambalo haliambatani na homa. Mara nyingi aina hii inaashiria uwepo wa tatizo katika ubongo inayosababisha mtiririko wa mawasiliano kati ya seli za ubongo wakati mwingine kuwa wa kasi kupita kiasi.

 

Degedege la namna hii huwa na tabia ya kujirudiarudia katika takribani nusu ya idadi ya watoto wanaopatwa nalo. Ni muhimu kupima viwango cha madini mwilini hasa sodium, sukari, au sumu katika damu. Iwapo litatokea mara mbili zaidi ya saa 24, hapo inaashiria tatizo la kifafa.

 

Degedege la watoto wachanga (Neonatal Seizure)

Hili huwapata watoto wachanga wenye umri chini ya siku 28 kwa sababu mbalimbali kama vile maambukizi ya vimelea viletavyo magonjwa, matatizo ya kimaumbile ya kuzaliwa nayo (Congenital structural abnormalities), sumu nk. Jinsi au namna wanavyopata degedege ni tofauti sana na watoto wengine kwa sababu degedege linalohusisha misuli ya mwili mzima halitokei kwa watoto wachanga.

 

Mara nyingi wanakuwa kama wanatafuna kitu, wakati mwingine macho kuyaelekeza upande mmoja bila ya kuyachezesha huku wakiwa wamekakamaa, pia wanaweza kuchezesha miguu kama wanaendesha baiskeli, lakini vilevile degedege linaweza kujionyesha kwa kubadilika rangi, au kutopumua kwa muda (apnea).

TIBA

Matibabu kwa watoto wadogo ni tofauti na watu wazima. Isipokuwa kwa sababu maalum na baada ya uchunguzi, watoto hawatakiwi kupata dawa pale wanapopata degedege kwa mara ya kwanza. Sababu ya kutowapa dawa mara ya kwanza wanapokwenda hospitalini ni madaktari wengi wanakuwa hawana uhakika kama lililotokea ni degedege au la. Dawa nyingi zina madhara makubwa kwa mtoto.

 

Mara nyingi huchukua wiki na zaidi au miezi kuizoea dawa na wakati mwingine inahitajika dawa zaidi ya moja kuweza kulikabili tatizo, hivyo uonapo dalili wahi hospitali akachunguzwe.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.