The House of Favourite Newspapers

Sallam SK: Harmonize Moyo Wake Hayupo Tena WCB

HATIMAYE uhakika wa taarifa za kuwa mkali wa Kwangwaru Harmonize hayupo tena katika Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) umethibitishwa na meneja wa kimataifa wa Diamond Platinumz, Sallam SK.

 

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Harmonize amejitoa katika Lebo ya WCB lakini palikosekana mtu wa kuthibitisha taarifa hizo.

 

Akizungumzia ishu hiyo, Sallam SK alisema: “Ni kweli Harmonize ameandika barua ya kuomba kujitoa katika Lebo ya Wasafi , hivyo sisi kama uongozi hatujaona kama hilo ni tatizo kwa sababu mwisho wa siku hauwezi kumzuia mtu kufanya kile ambacho anaona kwake kina manufaa zaidi.


“Wasafi ni kampuni na ina utaratibu wake, tutakaa kikao cha viongozi wote na yeye mwenyewe akiwepo ili kupitia ile mikataba ambayo tuliingia naye na kuona namna gani tutamalizana naye kwa kuwa kanuni zipo wazi, yule anayevunja mkataba ndiye inabidi alipe kama kutakuwa na gharama zozote kwenye ule mkataba.

 

“Kwa sasa moyo wake haupo tena WCB, Harmonize amebaki kwenye makaratasi tu mpaka hapo tutakapokaa na
kumalizana vizuri,” alisema.

 

Gazeti la Championi Ijumaa lilimtafuta mmoja wa meneja wapya wa Harmonize anayefahamika kwa jina Mchopa ambaye alisema: “Siwezi kulizungumzia hilo suala kwa sasa, siyo mimi wala mtu yeyote ambaye anaweza kusema lolote kuhusiana na ishu ya Harmonize kwa kipindi hiki.”

Comments are closed.