The House of Favourite Newspapers

KMC Inahitaji Sapoti ya Watanzania Leo Uwanja wa Taifa

LEO Ijumaa, KMC itakuwa na mchezo muhimu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Kigali ya Rwanda. Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Huu ni mchezo wa marudiano wa michuano hiyo baada ya ule wa awali uliochezwa takribani wiki mbili zilizopita kule Rwanda kumalizika kwa timu hizo kutofungana.

Kinachotakiwa kufanyika ni Watanzania wote bila ya kujali itikadi za kishabiki kuwa wazalendo na leo Ijumaa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia KMC iweze kufi kia malengo.

 

Ni rahisi kukuta mechi ya Simba, Yanga au Azam FC mashabiki kuwa wengi uwanjani, lakini upande wa KMC ni nadra sana, Ushindi wa aina yoyote leo utaipa nafasi KMC kusonga mbele hatua ya kwanza kwani hivi sasa ni mchezo wa hatua ya awali.

 

KMC ni timu changa kulinganisha na Azam FC, Simba na Yanga, hivyo haina mashabiki wengi ambao unaweza kusema wanaweza kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa ile sapoti kubwa.

hivyo nguvu ya Watanzania inahitajika kwao. Viingilio vya mechi hiyo inayotarajiwa kuanza saa 9 alasiri vimewekwa wazi. Kuna Sh 2,000 na Sh 5,000.

 

Ni viingilio ambavyo vinatoa nafasi kwa Watanzania wengi kuvimudu. Championi tunaungana na Watanzania wote kwa jumla kuiombea KMC na wawakilishi wetu wote waweze kufanya vizuri katika mechi zao za marudiano katika michuano hii ya kimataifa.

 

Wawakilishi wengine ambao ni Azam FC, wao watacheza kesho Jumamosi kama ilivyo kwa Yanga, lakini Simba mechi yao ni Jumapili. Itapendeza kuona wote wakishinda mechi zao hizo na kusonga mbele.

Comments are closed.