The House of Favourite Newspapers

Samatta Atangaza Kuwazima Liverpool Leo

 

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya KRC Genk, amefunguka kuwa atahakikisha anapambana kuwafunga Liverpool katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Leo Jumatano Samatta anatarajia kuiongoza Genk ya nchini Ubelgiji kucheza dhidi ya Liverpool katika mchezo wa tatu wa Kundi E linaloongozwa na Napoli yenye pointi 4, ikifuatiwa na Liverpool na Red Bull Salzburg ambao wote wana pointi tatu huku Genk ikiwa mkiani na pointi moja.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, baba mzazi wa mshambuliaji, mzee Ally Samatta alisema kuwa mtoto wake amejipanga kufanya vizuri katika mchezo huo ili kurahisisha ndoto yake ya kwenda kucheza ligi ya Uingereza.

 

“Binafsi nimeongea naye, amenihakikishia atafanya makubwa katika mchezo wao na Liverpool ambao utapigwa kesho (leo), Jumatano pale Genk kwa sababu mwenyewe akili yake yote ipo kwa yule beki bora wa dunia, Virgil van Dijk.

 

“Unajua hata mimi nimemueleza kwamba anatakiwa apambane haswa ikiwezekana yeye ndiyo acheze vizuri kuliko washambuliaji wote na amenihakikishia anamuonyesha van Dijk ubora wake kwa kuwa alishindwa kufanya hivyo kwa Kalidou Koulibaly wa Napoli kutokana na kumfahamu wakati wa Afcon kule Misri,” alisema mzee Samatta.

Stori na Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Comments are closed.