The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Ahimiza Wanawake Kufikia Hamsini Kwa Hamsini -Video

0

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wanawake wote nchini kuhakikisha wanamuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuaminika zaidi na kulifikia lengo la usawa wa asilimia kwa hamsini katika nyanja zote.

 

Rais Samia amezungumza hayo leo kwenye mkutano maalum ulioandaliwa mahususi kwa ajili ya kiongozi huyo wa nchi, kuzungumza na wanawake katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.

 

“Uwiano wa jinsia katika vyombo vya maamuzi na mfano halisi ni mimi niliyesimama hapa, miaka 20, 25 nyuma hatukulitarajia jambo hili kwamba tunaweza tukapata rais mwanamke.

“Mbele yetu tuna jukumu la hamsini hamsini, tusipofanya vizuri hatutafika huko. Tukolezeni rangi sasa hivi tuko kwenye kiti, twende tukoleze rangi tuaminike zaidi,” alisema Rais Samia.

 

Alisema, baada ya nchi kumpoteza aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli na yeye kuchukua nafasi ya urais kwa matakwa ya kikatiba, amejitahidi kwenye suala zima la kuhakikisha wanawake wanashika nyadhifa mbalimbali ili kufikia usawa na wanaume.

“Nilipoingia kwenye nafasi ya urais, nimefanya teuzi zifuatazo, makatibu tawala 26 ambapo kati ya hao, 12 ni wanawake. Ni sawa na asilimia 46 hivyo kwenye eneo hilo tunasogea kwenye asilimia hamsini,” alisema Rais Samia na kuongeza.

 

“Kwa upande wa mahakama tuliteua majaji 28 ambao kati yao, majaji kati 12 au 13 ni wanawake sawa na asilimia 43 hii nayo hatuko mbali kuifikia asilimia hamsini.”

 

Rais Samia aliongeza kuwa, hata Bungeni, mafanikio kwa wanawake yameonekana.
“Bungeni kwa kipindi cha pili tumekuwa na naibu spika mwanamke na pia tuna ongezeko la waheshimiwa wabunge wanawake.

“Kwa mara ya kwanza kwenye historia nimeteua katibu wa Bunge mwanamke, hii inanipa matumaini kwenye miaka michache ijayo tunaweza kufika usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya maamuzi,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alichukua nafasi hiyo pia kuwashukuru wanawake kwa kuwachagua yeye pamoja na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Magufuli.

 

“Niwashukuru wanawake wote kwanza kwa kumchangua hayati Dk John Pombe Magufuli katika uchaguzi uliopita na mimi kuwa Makamu wa Rais, uamuzi wenu ndio umenifanya kuwa Rais kwa matakwa ya kikatiba.

 

“Wanawake ni chachu ya maendeleo katika taifa lolote, hakuna taifa lolote linaloweza kupata maendeleo bila kuwategemea wanawake kwa sababu wanawake ni taifa kubwa,” alisema Rais Samia.

Rais Samia aliwataka wanawake waliopo kwenye nafasi mbalimbali, kuzitumia vizuri nafasi walizonazo ili kuwatengenezea mazingira mazuri wale wanaokuja kushika nafasi hizo.

 

Katika lengo la kuweka nguvu zaidi kwa kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora, Rais Samia alisema, Serikali imekusudia kujenga shule na mabweni kwa ajili ya wanawake.

 

“Kuanzia mwezi Julai mwaka huu, tutaanza mradi wa kujenga mradi wa shule moja ya sekondari yenye mabweni kwa kila mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wanawake,” alisema Rais Samia.

 

Pia, aliwataka wanawake kutumia vizuri fedha ambazo zinatolewa kama mikopo kutoka kwenye mifuko mbalimbali akitolea mfano wa majukwaa aliyowahi kuyaanzisha miaka ya nyuma.

“Katika kutimiza majukumu yangu kwa hapa nchini nilibuni wazo la kuanzisha majukwaa ya uwezashaji ya wanawake kiuchumi, madhumini ya majukwaa hayo ni kuwakutanisha wanawake kujadili fursa.

 

“Katika wakati ule, jumla ya majukwaa 23 yaliundwa katika ngazi ya mikoa, nafarijika kuona mpaka sasa majukwaa 18 kwa takwimu bado yapo na yanaendelea,” alisema Rais Samia na kuongeza.

 

“Ndani ya ofisi ya rais kulikuwa na mfuko wa kujitegemea, nikasema nitatutimia mfuko huu huu kulea majukwaa, naomba sana majukwaa ambayo yapo hai simameni vyema najipanga kuyasimamia na kuyalea majukwaa haya.”
Kwenye hotuba yake, Rais Samia alikiri bado kuna changamoto kwa wanawake katika suala zima la kumiliki ardhi lakini akawataka kukaa chini kwa pamoja na kuona namna ya kutatua changamoto hiyo.
“Kwa mfano ni asilimia 7.4 ya wanawake ndio wanaumiliki wa nyumba ya peke yao ukilinganisha na asilimia 25.6 ya wanaume,” alisema Rais Samia.

 

Kuhusu kuboresha huduma za afya hususan za uzazi, Rais Samia alisema anashukuru kuona wanaendelea vizuri na kwamba anafarijika kuona kwenye wizara hizo nyeti ambazo amewakabidhi wanamama na wanafanya kazi vizuri.
“Hili la kudaiwa mgonjwa akiwa amefariki, naomba muweke mpango mzuri wa kulishughulikia.

 

Uwepo utaratibu mzuri wa kulipa wakati mgonjwa akiwa anauguzwa na sio kudai kwa kuzuia maiti,” aliagiza Rais Samia.

Rais Samia alisisitiza jamii nzima kuachana na mfumo hasi wa kudhani wanawake hawawezi.
“Nahimiza jamii nzima kuachana na mtazamo hasi kuhusu wanawake, wanawake sio viombe dhaifu, wanawake ni viumbe imara.

“Tunabeba viumbe na kuwaleta duniani, kwa hiyo ni nguvu ambayo Mungu alitupendelea wanawake wanaume hawakupewa nguvu hiyo.

“Nguvu za kubeba magunia na nini Mungu hakutupa, sisi mwisho wetu midomo mikali kweli lakini ukiambiwa sogea hapa, mbio,” alisema Rais Samia.

Aliwataka wanawake wote nchini kuungana ili kuhakikisha wanawake wanazidi kuaminika zaidi katika jamii.
“Hili jungu la maji ya moto siko peke yangu, wanawake wote wa Tanzania tupo kwenye hili jungu. Kwa nini nasema hivyo, nasema hivyo kwa sababu, kwenye hili jungu la maji ya moto, tukiweka rangi tukiikoleza wanawake tuna nafasi nyingine mbele ya kuaminiwa,” alisema Rais Samia.

Mwishoni, Rais Samia aliwataka wanawake kutosahau majukumu yao katika familia. “Pamoja na jitihada kubwa tunazozifanya za kutaka usawa na uwezeshaji wa jinsia yetu, tusisahau majukumu yetu ya kulea familia na jamii kwa ujumla, mwanamke ni mzazi ni mama. Mwanamke ni mlezi wa watoto na baba wao watoto.

“Mwanamke ni mwalimu, mwalimu wa familia na majirani wanaokuzunguka kwenye kundi. Mwanamke ni muuguzi, anapoumwa mtu unaambiwa sasa jitayarishe basi nenda kamtizametizame, hasemi mimi nakwenda ngoja nikamtizametizame aaa, na kama atatangulia akirudi atakwambia fanya uende anaumwa ana homa kali, nenda basi,” alisema Rais Samia.
Stori: Erick Evarist, GPL

 

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP:
⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8
⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Leave A Reply