The House of Favourite Newspapers

Sanchoka Kupika Tu Hujui, Nani Atoe Mil 10 Ya Mahari?

0
Sanchoka au Sanchi.

NIMEWAHI kuandika mara kadhaa kuhusu huyu dada mwenye mvuto, hasa kwa wanaume wakware, Jane Limoy au kama mwenyewe anavyopenda afahamike sana kama Sanchoka au Sanchi.

 

Ni miongoni mwa wanamitindo matata Bongo, mojawapo ya kitu kilichompatia ‘headlines’ kubwa, ni ile kauli yake maarufu kuwa mtu anayehitaji kumuoa ni lazima ajiandae kwelikweli, kwani ‘hachomoki’ kwa wazazi wake bila milioni kumi, ambazo ni mahari pekee, kabla ya kitu kingine chochote.

 

Nimewahi kuonana mara moja na Sanchi na kwa kweli, kwa wanaume wenye kupenda wanawake wa aina yake, huyu ni bonge moja la mtoto, ambaye mwenye ‘kisu’ chake matata, milioni kumi si kitu kabisa.

 

Lakini wakati tamko lake hilo kuhusu kiasi cha mahari anachoweza kukubali ili mwanaume amchukue likiwa bado halijapoa, ameibuka na ishu nyingine akidai kuwa mazingira aliyokulia, yalimnyima fursa ya kujua kupika ugali, chakula maarufu zaidi kuliko vyote katika jamii ya wabongo.

Akabainisha kuwa angalau anaweza kujaribu kula, lakini kupika hajawahi kabisa. Kwa kuwa mimi ni miongoni mwa mashabiki wake, nimejikuta nikiijadili kauli hii na kujiuliza maswali mengi yanayokosa majibu.

 

Huenda kwa kuwa siifahamu historia ya maisha yake, maana huwezi kujua, unaweza kuwa unamuona mtu ukadhani wote mmekuja mjini na mfuko wa rambo, kumbe mwenzako alidondoka na Air France akitokea ughaibuni alikozaliwa.

 

Maana kuna baadhi ya nchi chakula chetu kikuu wao hawakifahamu kabisa, ingawa ni vigumu kidogo kwa Mtanzania aliyezaliwa hapa, akamudu kuishi huko ughaibuni bila kujipikia vyakula vya nyumbani, kwani washikaji ambao wapo huko wanatuambia jinsi gani wanavyobeba unga wa ugali, pindi wakirejea huko kutoka Bongo.

 

Hata pamoja na kutoijua vizuri historia yake, nilicho na uhakika nacho ni kuwa Sanchi amekaa muda mrefu hapa nchini kiasi kwamba kauli ya kutojua kwake kupika ugali lazima iwe ni ya kushangaza.

 

Na inashangaza zaidi anaposahau kuwa sokoni, tayari amejithaminisha kwa dau la shilingi milioni kumi kwa mwanaume anayetamani kumuoa, sasa unajiuliza, hiviaolewe na Msukuma (watani zangu) mwenye mihela yake kwa mfano, halafu uwe hujui kupika ugali, hivi kutakalika kweli ndani? Nadhani Sanchi aliongea hivyo kufurahisha genge au pengine kwa kufikiri ni kauli ndogo tu ambayo haina madhara.

 

Hii ni kauli mbaya kupita maelezo ambayo mwanamke wa kibantu anaweza kuiongea mbele za watu kuliko anavyodhani. Sasa kama hajui kupika ugali, vipi kuhusu maharage, yanayokaa jikoni zaidi ya saa moja? Inawezekana pia aliamini kwa kusema hivyo, atakuwa anawakoga akina Shilole ambao ni mama ntilie, wanaopika ugali kila siku, labda akiwaona washamba.

 

Nimsaidie huyu binti, moja kati ya vitu vinavyowaangusha akina dada wengi ni kudhani kuwa uzungu mwingi ndiyo utawafanya waonekane wa maana na wenye thamani.

 

La hasha, unapojiona kuwa ni mzungu zaidi kuliko mbantu, ndivyo unavyoziba nafasi ya watu kukuona kama mtu mwenye kufaa kuitwa mke. Sasa kama leo binti wa Kitanzania anasimama na kusema hajui kupika ugali, vipi kuhusu mlenda, ile mboga tamu ya asili?

 

Mtu ambaye hafahamu namna ya kusonga ugali, anaweza kweli kujua kuna makande yanaliwa? Siyo kila wakati ni wa kuishi kimaigizo, upo umuhimu wa muda mwingine kuwa kama kabila lako linavyotaka, yaani kama unaposalimia wanaume unapiga magoti na upige, siyo unaleta uzungu ambao haukusaidii kitu chochote zaidi ya kukuchoresha. Unaweza kuwa na figa bomba, rangi ya kupendeza na kila kitu kizuri, lakini kichwa kinapokosa kujua nini cha kusema na kwa wakati gani, kinatia dosari uzuri wote.

NA OJUKU ABRAHAM, ZA CHEMBE LAZIMA UKAE

Leave A Reply