The House of Favourite Newspapers

Sangoma Awafanyia Watoto Tukio Baya

MGANGA wa kienyeji ‘sangoma’ ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja na wateja wake, Peter Msambili na Zawadi Juma wanashikiliwa na Polisi baada ya kudaiwa kushirikiana kuwafanyia ukatili wa kuwaunguza mikono kwa maji ya moto watoto wawili (majina yao yanahifadhiwa kwa sababu ya kimaadili),wakati akifanya uganga wake.

 

Tukio hilo lilitokea Mei 25, mwaka huu ambapo Peter na Zawadi ambao ni wakazi wa Vingunguti-Butiama jijini Dar, waliwaachia chumba watoto hao wawalindie wakati wao wakiwa kazini usiku.

Chanzo cha habari hizi kimedai kuwa ilipofika asubuhi Zawadi na Peter waliporudi kwenye chumba chao walibaini kuwa fedha za Zawadi, kiasi cha shilingi 45,000 alizokuwa amezificha kwenye chumba hicho hazipo.

 

Baada ya kubaini kuwa fedha hizo zimepotea katika mazingira ya utata, waliwatafuta watoto hao ili wawaulize lakini wakawa wameshaenda kwa wazazi wao ambako si mbali na nyumba hiyo.

Zawadi na Peter waliamua kuwafuata watoto hao mpaka kwa wazazi wao na kumkuta baba yao aitwae GoodLuck Madagascar ambapo walimueleza upotevu wa fedha hizo.

Baada ya kumpasha tukio hilo, Zawadi na Peter walimuambia kuwa walikuwa wakiwahitaji watoto hao waende nao kwenye chumba hicho wakazitafute fedha hizo kwa pamoja huenda walizichukua na kuzihifadhi sehemu nyingine ndani humo.

 

“Baba huyo kwa kuwa Zawadi na Peter nao ni vijana wake wanaomuita mjomba, hakuwa na wasiwasi nao akawaruhusu watoto hao. Mmoja ambaye ni mwanaye na mwingine mtoto wa kaka yake waende kuwasaidia kuwatafutia pesa hizo,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliendelea kudai kuwa kumbe wawili hao walipowachukua watoto hao, walienda nao kwa mganga wa kienyeji (sangoma) aliyeko maeneo ya Tandale Kwa Tumbo jijini Dar kwa ajili ya kuwapa kibano watoto hao ili waseme kama wameiba fedha hizo au la.

 

Walipofika kwa mganga huyo aliwauliza watoto hao kama wameiba au hawakuiba fedha hizo, wakasema hawakuiba.

Chanzo kilisema sangoma huyo imedaiwa kuwa aliwaambia watoto hao kuwa anachemsha maji ya moto na itabidi waingize mikono maji yakiwa yanachemka na endapo hawahusiki na wizi wa pesa hizo hawataungua lakini kama wao ndiyo walioiba wataungua.

 

Imeelezwa kuwa maji yakiwa yanachemka Zawadi na Peter kwa kushirikiana na sangoma huyo walianza kuwalazimisha watoto hao kuingiza mikono kwenye maji hayo, wakakataa huku wakiendelea kukanusha kuiba fedha hizo, lakini sangoma huyo na wenzake hao waliwalazimisha kuingiza mikono ambapo alianza na mmoja ambaye baada ya kuingiza mikono tu aliungua mikono yake na akaangusha kilio.

 

Wakati wa kwanza ameshaunguzwa mikono, mwingine naye alilazimishwa kuingiza mikono, lakini akakubali kuwa ameiba ili asalimike kuunguzwa lakini wakiwa wanataka kuondoka alikataa na kusema hajaiba hivyo ikabidi wamkamate tena kwa nguvu na kumwambia achovye mikono yake kwenye maji ya moto, akachovya mmoja na kuungua kisha kuangua kilio.

Kufuatia tukio hilo mwandishi wetu alikwenda mpaka nyumbani kwa wazazi wa watoto hao na kumkuta baba wa watoto hao aliyejitambulisha kwa jina la Goodluck Madagascar ambaye alikuwa na haya ya kusema:

 

“Peter na Zawadi hawa wote wananiita mjomba na wamekuja hapa mjini wamefikia kwangu mpaka wanaanza maisha lakini kitendo walichowafanyia wanangu kimeniumiza sana roho yangu. “Wao wanafanya kazi kwenye machinjio ya Vingunguti sasa kwa kuwa kazi yenyewe wanafanya usiku hivyo walikuja hapa nyumbani kuniomba niwape hawa wadogo zao wakawalindie chumba chao.

 

“Siku ya tukio hawa watoto walirudi nyumbani asubuhi kama kawaida yao wakishatoka kuwalindia chumba chao, baada ya muda ndiyo nikawaona Zawadi na Peter wanakuja na kuniambia eti hawa watoto wamewaibia pesa zao walizokuwa wamezificha kwenye hicho chumba.

“Niliwauliza hawa watoto na kuwaambia kama kweli wamechukua si tabia njema wazirudishe haraka lakini walikataa katakata.” Aliongeza kuwa baada ya watoto kukataa waliomba wawachukue ili wakasaidiane kuzitafuta.

 

“Kumbe hawakwenda kwenye hicho chumba bali waliongoza moja kwa moja mpaka kwa sangoma ambaye amewaunguza hivi wanangu,” alisema baba huyo. Aliongeza kuwa alipoona watoto wanachelewa kurudi alidhani labda wamepelekwa Kituo cha Polisi cha Vingunguti akawafuatilia lakini hakuwakuta.

Alisema, alipiga simu akaambiwa wapo kwenye Baa ya Mashujaa, Vingunguti na alipowafuata akawakuta wameunguzwa mikono.

 

Alifafanua kuwa aliomba msaada kwa wasamaria wema watu hao wakamatwe na wakakamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Buguruni ambapo waliwaonesha polisi alipo sangoma na akakamatwa na kufunguliwa jalada lenye namba; BUG/ RB/3785/2018 KUJERUHI NA KUDHURU MWILI.

Mwanahabari wetu alizungumza na mmoja wa watoto hao ambaye alisema: “Nilishangaa sisi peke yetu ndiyo tuliambiwa tuingize mikono kwenye maji yanayochemka, eti kama tumeiba hizo pesa tutaungua wakati ilibidi na wao tuone wanavyoingiza mikono yao bila kuungua kwa kuwa hawakuiba,” alisema mmoja wa watoto hao.

STORI: RICHARD BUKOS, DAR.

Comments are closed.