The House of Favourite Newspapers

Serikali Yamwaga Bil 15 Kunusuru Soko la Mahindi ya Wakulima – Video

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeshatoa Sh15 bilioni kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kununua mahindi kutoka kwa wakulima.

 

Hatua hiyo inaweza kuwapa ahueni wakulima ambao wamekuwa na malalamiko ya kuwa na mahindi mengi yaliyokosa soko na hivyo kuwaweka katika hatari ya kupata hasara.

 

Majaliwa ametoa kauli hiyo jana Septemba 2, 2021 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kwela, Deus Sangu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

 

“Uzalishaji wa mahindi ni mkubwa lakini na sisi pia tumeimarisha hifadhi yetu ya Taifa ya chakula (NFRA) tumeipa fedha za kwenda kununua mahindi kwa bei ya kumuwezesha mkulima ili ajikimu hadi msimu ujao. Uwezo si mkubwa sana, lakini tumeipa Sh15 bilioni,” amesema Majaliwa.

 

Aidha, Waziri Mkuu amesema alipokuwa ziarani mkoani Katavi aliona hali halisi ya mlundikano wa mahindi na akakutana na watu wa NFRA ili aone kasi ya ununuzi ikoje.

 

“Nilibaini kuwa uwezo wao ni mdogo na nikapokea malalamiko ya wananchi kwamba kituo cha kupokelea mahindi kiko mbali, kwa hiyo tumeamua kuanzia sasa kila halmashauri itapaswa iwe na kituo japo kimoja cha kupokelea mahindi ili kuharakisha ununuzi wa zao hilo,” amesema Majaliwa.

 

Amewahakikishia wakulima kuwa Serikali itanunua mahindi kupitia NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko na kuwa kuwa Serikali imefungua milango kwa yeyote anayetaka kuuza mahindi nje ya nchi.

 

Mei 2021, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alitolea ufafanuzi wa suala la kununua mahindi kwa wakulima na aliainisha kuwa kwa wakati huo NFRA haikuwa na uwezo wa kununua mahindi ya wakulima lakini ipo mikakati inayofanyika kufungua soko la zao hilo nje ya nchi.

 

Hatua hiyo ya Serikali huenda ikawapa ahueni wakulima ambao wan a akiba kubwa ya mahindi kwenye maghala.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Global Publishers (@globalpublishers)

Leave A Reply