Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu akiongea na wakazi wa Mwanza.
Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), Sarafina Mkuwa akiwataka akina mama na mabinti mkoani Mwanza kujitokeza kwa wingi katika upimaji wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
Makamu wa Rais, Samia Hassan akiteta jambo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti Mwanza.
Wananchi waliojitokeza kupima saratani katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
Baadhi ya manesi wakiwa kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Angelina Mabula akiongea na wakazi wa Mwanza.
JUMLA ya Sh. Bilioni 7 zimetengwa na serikali ili kukabiliana na magonjwa ya saratani ambayo yamekuwa yakichangia kwa kiasi kukubwa vifo vya kina mama na mabinti. Hii ni kutokana na watu hao kupoteza maisha kwa ugonjwa huo kwa kukosa fedha za matibabu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha upimaji wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa akina mama na mabinti jijini hapa jana, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, alieleza kuwa mwaka jana serikali ilikuwa imetenga Sh. Billion moja na kwamba kwa sasa kiwango hicho kimeongezwa ili kukabilina na vifo vitokanavyo na magonjwa hayo sugu.
“Tumejitahidi kwa kiasi kikubwa katika serikali hii ya awamu ya tano kuhakikisha tunaboresha afya ya mama na mtoto lakini pia kuhakikisha tunasaidia kutibu magonjwa hayo sugu ambayo yanaendelea kuwa tishio kwa wanawake hasa kwenye nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania”, alisema Samia.
Aidha aliwapongeza madaktari wote nchini katika kujitoa na kuhakikisha wanaokoa maisha ya Watanzania katika sekta zote kama macho, migongo-wazi, moyo na kuwataka kuendelea na moyo huohuo licha ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Aliongeza kuwa serikali imetoa kipaumbele kwa magonjwa hayo kutokana na idadi ya wangojwa wa saratani ya mlango wa kizazi kufikia asilimia 38, huku saratani ya matiti ikiwa ni asilimia 12, saratani ya koo ikiwa na asilimia tisa, kichwa na shingo 7, matezi 5.4, damu 4.7 na kibofu cha mkojo asilimia tatu.
Alieleza kuwa aidha serikali haijasahau magonjwa ya tezi dume kwa wanaume kutokana na kwamba ndani ya mwezi mmoja wanaume saba waliobainika kuwa na ugonjwa huo wanne wamefariki dunia.
Awali Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), Sarafina Mkuwa, aliwataka kina mama na mabinti mkoani hapa kujitokeza kwa wingi katika upimaji wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi ili watakaogundulika waaze matibabu haraka.
“Ugonjwa huu unatibika ukiwahi kupima na kugundulika hivyoa niwatake kina mama wenzangu wapunguze unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara, kuwa na wapenzi wengi na kuanza mapenzi katika umri mdogo kuwa ndiyo uchangiaji mkubwa wa kirusi kiitwacho Human Papromal (HPV).
Aidha alivitaja vituo vinne vitakavyokuwa vinatoa huduma kwa siku mbili jijini hapa kuwa ni Furahisha, Makongoro, Igoma na Karume lengo lake kubwa likiwa ni kupima kina mama 3,000 upande wa saratani ya matiti na 1,200 saratani ya mlango wa kizazi.
Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Leornad Subi, alisema kuwa mwaka jana kati ya wagonjwa 1,6000 waliofanyiwa uchunguzi wa awali, 333 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo, ambapo 185 wakipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando na 66 wakiwahishwa kwenye Hospitali ya Ocean Road.
Na Idd Mumba, Mwanza
Comments are closed.