Waziri Kairuki Akutana na Rais wa Apimondia Kamisheni ya Afrika
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Apimondia Kamisheni ya Afrika, Bw. David Mukomana kwa lengo la kujadili maandalizi ya mkutano wa 50 wa Dunia wa Ufugaji Nyuki (APIMONDIA) na kuweka mikakati ya kufanikisha mkutano huo utakaofanyika nchini mwaka 2027.
Akizungumza katika kikao hicho, kilichofanyika leo Aprili 29,2024 jijini Dodoma, Waziri Kairuki amemuhakikishia Bw. Mukomana kuwa Serikali ya Tanzania imejipanga vizuri kufanikisha mkutano huo ikiwemo maandalizi ya ukumbi, utangazaji na masuala mengine ya muhimu.
“Nataka niwahakikishie kwamba Tanzania itafanya kazi usiku na mchana kwa ukamilifu, bila kuchoka kwa kushirikiana na uongozi wa Apimondia katika kipindi chote cha maandalizi ya mkutano huu” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Vilevile Mhe. Waziri ameeleza kuwa, mkutano huo ni muhimu sana hasa katika Sekta ya Ufugaji Nyuki ambapo utatoa fursa ya kuelimisha umma na kuhamasisha kizazi cha sasa na kijacho kushiriki katika shughuli ufugaji nyuki.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amesema Tanzania itahakikisha inaendeleza sekta ya ufugaji nyuki huku ikitambua umuhimu wa Sekta hiyo kwenye mchango wa ajira hasa kwa vijana na wanawake pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Aidha ,Mhe. Kairuki ametumia fursa hiyo kumualika Bw. Mukomana pamoja na Rais wa Apimondia, Dkt. Jeff Pettis kuhudhuria Maonesho ya Asali (Honey Show) yatakayofanyika nchini tarehe 19-21 Juni mwaka 2024.
Kwa upande wake, Bw. Mukomana amesema mojawapo ya mikakati inayotakiwa kukamilishwa kuelekea Mkutano wa 50 Apimondia ni kuhakikisha kunakuwa na ushiriki mkubwa wa wadau wa ndani na nje ya nchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof.Dos Santos Silayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Daniel Pancras pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.