The House of Favourite Newspapers

SGA Yapokea Tuzo kwa Ulipaji Kodi Bora

0
Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Bw. Eric Sambu.

 

KAMPUNI ya SGA Security ambayo, ndio kampuni kongwe binafsi ya ulinzi nchini, imepokea tuzo kutoka kwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) kufuatia mwenendo wake mzuri wa ulipaji kodi. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla maalumu iliyoandaliwa na TRA ili kuwatambua walipa kodi bora.

 

SGA ilishika nafasi ya tatu jumla katika kundi la walipa kodi wakubwa kwa eneo la Tegeta. Vigezo vilivyotumika katika kutoa tuzo hizo ni pamoja na kiasi cha kodi, uwazi, ulipaji kwa wakati na ushirikiano kwa maafisa wa TRA.

Waziri wa Habari na Mawasiliano, Mh. Nape Nnauye.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Bw. Eric Sambu alisema tuzo hiyo ni ya kipekee hasa ikizingatiwa inatoka TRA.  “Ni wajibu wetu kulipa kodi na tuzo hii inadhihirisha mwendendo wetu mzuri katika hili. Leo tunaadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa kampuni yetu, Marehemu Edmond van Tongeren, kwa hivyo tuzo hii ni heshima kubwa kwake kwani inadhihirisha urithi mzuri ambao aliacha kwa makampuni yetu yote,” alisema;

 

Pamoja na tuzo hii ya TRA, kampuni ya SGA pia ilipokea tuzo nyingine hivi karibuni ya mtoa huduma bora na salama anayekubalika na wateja na mwenye kutumia vifaa bora na vya uhakika katika kutoa huduma ukanda wa Afrika Mashariki. Kampuni hiyo yenye wafanyakazi zaidi ya 6000 nchi nzima pia ilipokea tuzo ya mwajiri bora Zanzibar.

Bw. Sambu alisema makampuni binafsi ya ulinzi yana mchango mkubwa sana kwa uchumi kwani yanasaidiana na polisi kuhakikisha sheria inafuatwa na wananchi wanakaa kwa amani.

 

Alitoa wito kwa makampuni mengine yaige mfano wa kampuni yake na wafanye biashara kwa kufuata utaratibu na pia kutoza bei sahihi ambazo zitawawezesha kuangalia masilahi ya wafanyakazi wao, kulipa kodi ipasavyo na pia kubakiwa na akiba ya kuwekeza zaidi katika biashara.

 

“Kuna vita vya bei sasa hivi na baadhi ya makampuni yanatoza bei ambazo haziwezi kufanya wajiendeshe kifaida lakini pia wanashindwa kulipa kodi,” alisema.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Habari na Mawasiliano, Mh. Nape Nnauye aliipongeza TRA kwa kubadilisha mfumo wake wa ukusanyaji kodi kwani imechangia katika kutimiza malengo ikiwa ni katika kutekeleza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati anazindua Bunge la sasa.

 

Waziri huyo alitoa wito kwa TRA iendelee kuwekeza zaidi katika teknolojia ili kuhakikisha walipa kodi wote wanafikiwa kwa urahisi na wanaendana na teknolojia. Aliongeza pia kuwa matokeo ya ukaguzi wa kodi yanatakiwa kuonesha uhalisia  ili pamoja na mambo mengine masilahi ya wafanyakazi yazingatiwe na biashara ziweze kuendelea bila tishio la kufunga.

 

Aliipongeza TRA kwa kuvunja kikosi maalumu cha kukusanya kodi ambacho hakikuwa na faida kwani biashara nyingi zililazimika kufunga.

Leave A Reply