The House of Favourite Newspapers

Sholo Mwamba Fundi Wa Kukaangiza, Mtaalam Wa Singeli

shalo-mwamba-2

Staa wa Muziki wa Singeli, Sholo Mwamba akiwa nyumbani kwake Bahari Beach, Kunduchi jijini Dar ambapo kwenye mjengo huo aliopanga, anaishi peke yake.

shalo-mwamba-3

Akiwa anachati na mashabiki zake katika Facebook.

shalo-mwamba-4

Akiandaa wimbo mpya.

shalo-mwamba-5

Akiandaa madikodiko ya kupika.

shalo-mwamba-6

…Akiosha vyombo.

shalo-mwamba-1

Akimwagilia maua maji.

NA IMELDA MTEMA/GPL

SEIF Mwinyijuma linaweza kuwa jina geni masikioni mwa Watanzania wengi lakini ukiwatajia Sholo Mwamba, wengi wanamfahamu kama staa wa Muziki wa Singeli. Leo Mpaka Home imemtembelea nyumbani kwake, Bahari Beach, Kunduchi jijini Dar ambapo kwenye mjengo huo aliopanga, anaishi peke yake.
Mpaka Home imezungumza naye mambo mengi kuhusu maisha yake ya nyumbani, twende pamoja:
Mpaka Home: Unaishi na nani kwenye nyumba kubwa hii?
Sholo Mwamba: Naishi peke yangu, yaani kisela tu.
Mpaka Home: Nyumba inaonesha ni kubwa sana unamudu vipi kufanya usafi?
Sholo Mwamba: Kwenye suala la usafi yaani hapo usinipimie hata kidogo, kwa sababu nishazoea, huwa nasafisha mwenyewe tu.
Mpaka Home: Ratiba yako ipoje kwa siku?
Sholo Mwamba: Baada ya kuamka huwa napiga tizi kwanza kuweka viungo sawa kisha nahamia kwenye usafi maana si unajua usela siyo uchafu kisha mengine yanafuata.
Mpaka Home: Suala la madikodiko, nani anayetengeneza?
Sholo Mwamba: Eneo hilo haruhusiwi mtu yeyote kwa sababu mimi mwenyewe ni fundi wa kukaangiza, hivyo sina haja ya kuomba nipikiwe au kununua vyakula kama baadhi ya mastaa wanavyofanya.
Mpaka Home: Starehe yako kubwa ukiwa nyumbani ni ipi?
Sholo Mwamba: Napenda kuandika mistari kama hivi unavyoona nina daftari na kompyuta mpakato (laptop) lakini ugonjwa wangu mkubwa ni kutazama muvi.
Mpaka Home: Hongera naona upo kwenye mjengo wa maana, umepanga au umejenga?
Sholo Mwamba: Hapa nimepangishiwa na menejimenti yangu inayosimamia shughuli zangu za muziki.
Mpaka Home: Unauzu ngumziaje Muziki wa Singeli, unakua au unasuasua?
Sholo Mwamba: Hapa tulipo ni hatua nzuri ukilinganisha na historia nzima ya muziki wetu kipindi cha nyuma, ambapo ulionekana kama wa kihuni. Sasa hivi kila mmoja ameukubali mpaka mshamba anaelewa. Naamini tutazidi kutoboa zaidi ya hapa.
Mpaka Home: Unamudu vipi ushindani uliopo baina yako na wasanii wenzako wa Singeli?
Sholo Mwamba: Unajua sisi kila mmoja ana ladha yake adimu ambayo inasababisha mashabiki wake wamkubali. Hata hivyo, sishindani na mtu.
Mpaka Home: Masela wako wa zamani, vipi wanakutembelea hapa?
Sholo Mwamba: Hahaa! Siwezi kuwakwepa wanangu kwa sababu wao nilikuwa nao kabla ya kutusua sasa naanzaje kuwatenga, nikifanya hivyo nitaonekana kama nimesaliti kambi.
Mpaka Home: Umesema unaishi peke yako, kwa hiyo huna mchumba?
Sholo Mwamba: Ninaye, ila kwa sasa sikai naye yupo kwao.
Mpaka Home: Mipango yenu ipoje yaani ndoa au vipi?
Sholo Mwamba: Mipango ipo na haitafutika hata kidogo, ila kwa sasa nakomaa kukuza muziki wangu utusue zaidi.

Comments are closed.