The House of Favourite Newspapers

Shehe Alhadi M. Salum: Kufunga siyo kujizuia kula tu

0

AlhadiMussaSalum (1)Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum amewatahadharisha wafungaji wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutorudia dhambi zao baada ya mfungo kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kumjaribu Mungu wakati hajaribiwi. Katika mahojiano maalum na gazeti hili pamoja na mambo mengine ametoa elimu kwa Waislamu na wasio Waislamu kuhusu mambo mbalimbali likiwemo suala la kuoana. Fuatana nasi katika sehemu hii ya kwanza ya mahojiano yetu:

Tunaomba ueleze maana ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa wanaofunga hata wasiofunga.

JIBU: Kuna watu wanadhani kufunga Ramadhani ni kujizuia kula tu, hapana, inatakiwa mfungaji achunge mipaka ya funga, yaani kujizuia viungo vyote. Ajizuie asiseme uongo, asitoe matusi, asisikilize milio haramu, pua isinuse vitu haramu kwa mfano, mwanamke asipake manukato kwa nia ya kumvutia mwanaume fulani, mikono ya mfungaji isitoe au kupokea rushwa, kupiga mtu, miguu isimpeleke sehemu kufanya maovu na kadhalika.

Ipo kawaida kwa baadhi ya Waislamu kuswali na kuhudhuria ibada misikitini wakati wa mfungo, baada ya hapo wanaacha, nini ushauri wako?

Jibu: Mwezi wa Ramadhani ni darasa kubwa la kutenda mema kwa Mungu, subra na kusameheana. Tuliyojifunza katika mwezi huu tunatakiwa kuyaendeleza. Uliyoyaacha yawe hivyo mpaka Ramadhani ingine na mfungaji ajiepushe kujiingiza kwenye tope. Wafungaji wanaorejea kwenye maasi baada ya mfungo wafikiri na wajue kwamba lengo lao la ucha Mungu halijatimia. Nashauri baada ya mfungo misikiti ijae kama inavyojaa sasa.

Kuna baadhi ya watu wana kawaida ya kufunga siku chache na kudanganya kuwa watalipiza siku sijazo lakini hawalipizi, nini ushauri wako kwa hilo?

JIBU: Jambo hilo limekemewa sana. Wapo wanaoacha kufunga kwa sababu nyepesi, mtu mwenye kufanya hivyo aelewe kwamba siku moja hiyo aliyosema atalipia, hailipiki hata alipe kwa mwaka mzima. Mtume Mohammed (SAW) anasema kuacha kufunga bila udhuru kama vile kuumwa na kadhalika ni mbaya hata kuliko mzinifu. Hilo ni jambo la haramu sana.

Kuna maelezo mitaani kwamba mtu akifunga basi futari na hata daku asipikiwe na hawara lakini wapo baadhi ya wafungaji huwa wanakwenda kufuturu kwenye biashara za wafuturishaji ambao ni hawara zao kwa madai kwamba pale wanakwenda kununua, unashauri nini hapo?

Jibu: Ni swali zuri.Mtu anayekwenda kufuturu kwenye biashara ya hawara yake funga haiharibiki kama anakwenda kununua futari kwa dhati kutoka moyoni. Mfungaji huyo akumbuke kuwa Mungu hadanganyiki. Kama anakwenda pale kwa mambo mengine ajue malengo yake ya swaumu hayafikii. Moyo wako ukikuambia kufanya hivyo ni dhambi basi ni bora kujitakasa na kuwa mbali na viashiria. Kama mpika futari huyo kabla ya Ramadhani alikuwa anazini naye ni bora kumkimbia kabisa ili moyo usiwe na wasiwasi. Nenda kafuturu kwingine mbali naye.

Jumanne ijayo Shehe Alhadi atajibu kuhusu kupanda pikipiki (bodaboda) na kumkumbatia dereva ni dhambi kwa mwanamke wa Kiislamu au si dhambi? Je, sahihi mtu kubadili dini kwa lengo fulani na akishalitimiza anarudi kwenye dini yake ya zamani na mtu huyo kuwa na tabia hiyo mara kwa mara kama wafanyavyo baadhi ya wasanii? Ataeleza pia tabia ya baadhi ya watu kufunga ndoa kwa mkuu wa wilaya ambapo amewakosoa viongozi hao wa serikali, Je ni kwa nini? Yote hayo na mengine mengi utayapata Jumanne ijayo. Usikose kupata nakala yako.

 

Leave A Reply