The House of Favourite Newspapers

SHEHE PONDA AKATAA SADAKA YA MONDI

0

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shehe Issa Ponda amesema msikiti uliojengwa na Supastaa wa Bongo Fleva; Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na kuutoa kama sadaka kwa waumini na viongozi wa kiislamu mkoani Kigoma, ni haramu. RISASI mchanganyiko linaripoti.   Hatua hiyo imekuja baada ya Desemba 30, mwaka jana, Diamond kuzindua msikiti huo alioujenga katika eneo la Ujiji, jambo ambalo lilizusha mijadala mizito ndani ya jamii ya Waislamu na katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Msikiti huo unaojulikana kwa jina la Masjidi Al Aziz ulizua mijadala kutokana na uhalali wa fedha zilizotumika kuujenga kutafsirika kuwa zimetokana na mapato yasiyo ya kimaadili kulingana na taratibu za dini hiyo na hasa kutokana na aina ya kazi anayoifanya msanii huyo.

Kutokana na hali hiyo, RISASI lilizungumza na Shehe Ponda ambaye kwanza alieleza kushangazwa na viongozi walioupokea msikiti huo na pia kumuombea dua Diamond ili abarikiwe kufanya tamasha lake vizuri.

Diamond alifanya tamasha mkoani humo Desemba 31 kama sehemu ya kuadhimisha miaka 10 ya uwepo wake kwenye sanaa. Shehe Ponda alianza kufafanua kuwa kiujumla jengo la msikiti huo kwa kuwa limeshakabidhiwa kwa madhumuni ya dini, viongozi hawawezi kulazimisha libomolewe hivyo ni halali kwa waumini kulitumia.

MAKUSUDIO YA MTOAJI

Hata hivyo, alienda mbele zaidi na kufafanua kuwa, kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, sadaka aliyoitoa Diamond haikubaliki kidini.

Alisema, kwa kuwa madhumuni ya mtoaji kwa jengo hilo ni kupata thawabu kwa Mwenyezi Mungu, sheria inaonesha hatopata kitu kwa sababu fedha yake imetokana na misingi ambayo si halali. “Matarajio yake kama ni kupata malipo kwa Mungu, hawezi kuyapata kwa sababu amekwenda kinyume chake… yaani amefanya kejeli.

“Kwa sababu amechuma kwa njia ambayo Mwenyezi Mungu ameikataza, alafu anasema anampa Mwenyezi Mungu, hiyo si sawa, hatapata malipo mazuri… atapata kinyume chake,” alisema. Ponda alimtuhumu Diamond kwa kupotosha umma pale aliposema pesa yoyote inayopatikana kwa njia isiyo ya halali kama vile biashara ya ukahaba au wizi, inaweza kutumika kujengea nyumba za ibada jambo ambalo si sahihi.

“Ndiyo maana tunakemea ule utaratibu wa kuhusisha pato haramu na Mwenyezi Mungu, kwa sababu hicho ni kitu ambacho si mafundisho mazuri kwa jamii,” alisema.

AWASHANGAA MASHEHE KIGOMA

Aidha, kiongozi huyo ambaye anaheshimika kwa waumini wa dini hiyo ndani na nje ya nchi, alishangazwa na kitendo cha mashehe wa mkoa wa Kigoma kwa kumuombea dua na baraka Diamond ili afanikiwe katika shughuli zake ikiwa tamasha la kufunga mwaka alilolifanya mkoani humo Desemba 31.

“Katika watu wa kulaumiwa ni wale viongozi wa Kiislamu ambao walithubutu kuonesha kuwa jambo lile ni zuri na kuliombea dua… wamekwenda kinyume kabisa na mafundisho ya Kiislamu na  maadili ya uongozi. “Wametoa mchango mbaya wa mafundisho katika jamii. Tunaomba waumini wasiyapokee, ule mtazamo wa viongozi wa dini pia wasiupokee kabisa,” alisema.

AWAASA VIONGOZI WA DINI

Aidha, Shehe Ponda alitoa wito kwa viongozi wa dini nchini kufanya tathmini ya misaada yote inayotolewa katika nyumba zao za ibada ili kujua kwa kina fedha hizo zimetokana na nini ili kukwepa uovu wa kuwapotosha watu.

“Wakigundua mtu huyo ameleta chumo ambalo si halali, wamsaidie kumbadilisha ili uchumi wake uwe halali. “Wanamuziki pia tunawashauri, waangalie kuwa wao ni kioo cha jamii, kwanza waangalie mziki wao unawaelekeza vijana kuwa weledi au lah… waangalie kuanzia mashairi yao, kama ni mabaya au ni mazuri. Na kama hawataki kubadilika basi wabakie hukohuko hadi pale watakapoamua kubadilika,” alisema.

WENGINE WAMTETEA DAMOND

Katika hali ambayo inaonesha kuwa na mgongano wa kiimani, baadhi ya watu wamekosoa msimamo wa wale wanaoamini kuwa kitu alichofanya Diamond kwa kujenga msikiti ni dhambi. “Kwanza mhukumu wa mwanadamu ni nani kama siyo Mwenyezi Mungu, wewe unaweza kujiona uko sahihi kwa sababu matendo yako unayaficha.

“Kuna mashehe wazinzi, kuna viongozi wa dini wezi, sasa nao tusemeje? Mimi mtazamo wangu ni kwamba mtu akifanya jambo jema au baya aachiwe Mungu ndiyo anayejua malipo yake na wala si binadamu,” alisema Ustadhi Hussein Jamal wa Magomeni jijini Dar es Salaam.

Stori: Mwandishi Wetu, DAR

Leave A Reply