The House of Favourite Newspapers

Shein Aipongeza China Kwa Kusaidia Maendeleo Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo sambamba na kukuza uhusiano uliopo. 

Dk. Shein amesema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China Cai Defeng, aliopo nchini Tanzania kwa ziara ya siku sita kufuatia mwaliko wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa Serikali ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzbar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo imekuwa chachu katika kukuza uchumi wa Zanzibar. Rais Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Jamhuri ya Watu wa China ambapo ujio wa kiongozi huyo unathibitisha ukweli huo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar alipongeza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya (CCM) na chama cha Kikomunisti cha China (CPC) chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping wan chi hiyo.

Dk. Shein alizipongeza hatua za Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo afya, elimu, kilimo, maji safi na salama, miundombinu, viwanda na mengineyo Dk. Shein alipongeza juhudi kubwa zinazochukuliwa na nchi hiyo katika kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Zanzibar sambamba na mashirikiano yaliopo kutoka Jimbo la Jangsu katika kuimarisha sekta ya afya.

Alipongeza azma ya Jamhuri ya Watu wa China kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo uchumi wa bahari, uvuvi, uwekezaji pamoja na gesi asilia na mafuta.

Dk. Shein aliwakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuekeza Zanzibar sambamba na watalii wa nchi hiyo kuitembelea Zanzibar kutokana na vivutio kadhaa vilivyopo hapa nchini. Rais Dk. Shein alieleza kuwa uchumi wa Bahari ni miongoni mwa mambo muhimu yaliopewa kipaumbelea na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi wake hasa ikizingatiwa kuwa ni mwa wanachama wa nchi zinazopakana na bahari ya Hindi (IORA).

Nae, Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China Cai Defeng alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.

Comments are closed.